Polisi wanasa bangi, heroine

06Mar 2017
Hamisi Nasiri
MTWARA
Nipashe
Polisi wanasa bangi, heroine

JESHI la Polisi mkoani Mtwara, limekamata kilo 74.14 za bangi na gramu 100 ya dawa za kulevya aina ya heroine.

Kamanda wa Polisi mkoani Mtwara, Neema Mwanga, alisema jeshi hilo linaendelea na operesheni dhidi ya dawa za kulevya na kwamba mpaka sasa watu 56 wamekamatwa kwa tuhuma za matumizi na biashara ya dawa hizo.

Kamanda Mwanga alifafanua kuwa kati ya watuhumiwa hao, 47 ni wanaume na wanawake tisa wakiwamo raia wawili wa Nigeria.
Alisema baadhi ya watuhumiwa hao tayari wamefikishwa mahakamani na kupatikana na hatia.

Kwa mujibu wa Kamanda Mwanga, waliopatikana na hatia, walihukumiwa vifungo vya kati ya miezi mitatu na sita ama kulipa faini ya kati ya Sh. 50,000 na Sh. 300,000 au vyote kwa pamoja.

Aidha, alisema watuhumiwa wanne ambao ushahidi ulionyesha kuwa wanajihusisha na biashara hiyo haramu, lakini hawakukutwa na dawa hizo, watakuwa chini ya uangalizi wa polisi huku wakichunguzwa mienendo yao.

Aidha, polisi mkoani humu wanashikilia pikipiki mbili mali za watuhumiwa hao zenye namba za usajili MC 489 BER na MC 424 ADL zinazodaiwa kutumika kusafirishia dawa na bangi hiyo iliyokamatwa.

“Operesheni hii ni endelevu vile vile tunatoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa zinazohusu biashara hii ya dawa za kulevya na uhalifu kwa jumla,” alisema Kamanda Mwanga.

“Taarifa hizo zitashughulikiwa kwa usiri mkubwa, lakini pia natoa onyo kuwa taarifa hizo ziwe ni za ukweli na sahihi ili hatua zinapochukuliwa asionewe mtu yeyote na kumbukeni kutoa taarifa za uongo, ni kosa la jinai,” alisema na kuonya Kamanda Mwanga.

Habari Kubwa