Polisi wanolewa kutenda haki

09Dec 2018
Romana Mallya
DAR ES SALAAM
Nipashe Jumapili
Polisi wanolewa kutenda haki

JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limetoa mafunzo ya kuwajengea uwezo maofisa wake ili kutenda haki na kusikiliza kesi kwa faragha zinapowafikia.

Kamanda wa Kanda hiyo, Lazaro Mambosasa.

Mafunzo hayo yamekuja ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto.

Kamanda wa Kanda hiyo, Lazaro Mambosasa, aliyasema hayo juzi wakati akifungua mafunzo hayo yaliyohudhuriwa na wadau mbalimbali wakiwemo Chama cha Wanasheria Tanzania (TAWLA), Ustawi wa Jamii na Dawati la Jinsia Polisi linaloshughulikia malalamiko ya ukatili wa kijinsia.

“Naendelea kuhamasisha watu wote wanaofanyiwa vitendo vya ukatili wasibaki navyo kwa sababu vina athari ya kisaikolojia, watoe taarifa Jeshi la Polisi kupitia madawati yetu yaliyopo vituo vya polisi ili zifanyiwe kazi,” alisema.

Mambosasa alisema mafunzo hayo yamelenga kujengeana uwezo wao kwa wao ili maofisa hao wasimamie sheria na haki itendeke.

“Mwanamke amelindwa katika kifungu namba 26 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai Sura ya 20 ambacho kilifanyiwa mapitio mwaka 2002, imeelekeza mwanamke anapokamatwa na kupekuliwa lazima akamatwe na mwanamke mwenzake,” alisema.

Kamanda Mambosasa alisema endapo akivamiwa na mwanaume tayari mtu huyo atakuwa ametenda shambulio la aibu na anapaswa kufikishwa mahakamani.

Ijumaa iliyopita, Kamanda Mambosasa alitoa ripoti ya vitendo vya ubakaji vilivyoripotiwa Jeshi la Polisi Kanda hiyo na kueleza kuwa katika kipindi cha miezi 10  ya mwaka huu, wanawake na watoto 714 wamebakwa.

Alisema kesi za ubakaji zilizoripotiwa polisi ni 714 na kati yake zilizopo chini ya upelelezi ni 539 na mahakamani ni 175 zikiwa na jumla ya watuhumiwa 158.

“Kesi za kulawiti zilizoripotiwa ni 229, zilizopo chini ya upelelezi 186, zilizopo mahakamani ni 43 zikiwa na jumla ya watuhumiwa 47,” alisema.

Naye, Mrakibu Msaidizi wa Polisi Helen Kaduri kutoka kanda hiyo, alisema Mkoa wa Dar es Salaam una madawati 22 yanayoshughulikia ukatili wa kijinsia.

Habari Kubwa