Polisi wasaka wauaji wa Watanzania Msumbiji

03Jul 2019
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe
Polisi wasaka wauaji wa Watanzania Msumbiji

JESHI la Polisi nchini kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi la Msumbiji, wanawasaka watu waliohusika na mauaji ya Watanzania tisa waliopigwa risasi na watu wasiojulikana nchini humo.

Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) David Misime.

Katika mauaji hayo yaliyotokea wiki moja iliyopita nchini Msumbiji, wako pia raia wawili wa Msumbiji ambao wote waliuawa katika kijiji cha Mtole.

Nipashe ilipomtafuta jana Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) David Misime, ili kujua hadi sasa kama kuna watu wamekamatwa kutokana na mauaji hayo, alithibitisha kufanyika kwa msako huo.

"Jeshi la Polisi Tanzania na Jeshi la Polisi Msumbiji yako kazini kuwasaka wauaji," alisema.

Ijumaa iliyopita, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Sirro, aliliambia gazeti hili kuwa mbali na vifo hivyo, wako pia majeruhi sita.

Alisema watu hao walivamiwa wakiwa kwenye mashamba yao ya mpunga na watu waliovalia sare zinazofanana na za Jeshi la Msumbiji.

IGP Sirro alisema siku hiyo kuwa juhudi za kuwasaka waliofanya mauaji na kujeruhi watu hao zinaendelea.

 "Ninawaambia wauaji kuwa damu ya Watanzania haiendi bure, walioua tutawasaka kwa kushirikiana na majeshi ya Msumbiji kuhakikisha tunawakamata wakiwa hai au wamekufa. Wahalifu hawa baada ya kufanya vurugu waliondoka na wanawake wawili wa Tanzania na mtoto mmoja na hadi sasa hawajapatikana," alisema.

Aliongeza kuwa: "Hawa Watanzania walikuwa Msumbiji wakijishughulisha na kilimo cha mpunga. Wakiwa kwenye mashamba yao ambako wameweka vibanda vya muda, ghafla walivamiwa na watu wakiwa wamevalia sare zinazofanana na za Jeshi la Msumbiji na kuwaua baadhi na wengine kuwajeruhi."

"Tumewatembelea majeruhi, wako Watanzania sita na wengine wawili ni raia wa Msumbiji wanaendelea na matibabu katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Mtwara ya Ligula," alisema.

Habari Kubwa