Polisi washutumiwa kila kona kipigo mwanahabari

11Aug 2018
Romana Mallya
DAR ES SALAAM
Nipashe
Polisi washutumiwa kila kona kipigo mwanahabari

UJUMBE wa video uliosambaa mitandaoni ukiwaonyesha askari polisi wakimpiga mwandishi wa habari kwa kumchangia, umeibua mjadala mkali kwenye jamii huku Jeshi la Polisi likitangaza kuanzisha uchunguzi na kuwahoji wahusika.

Mwandishi huyo, Silas Mbise, wa kituo cha redio cha Wapo FM, alipigwa na askari hao siku ya tamasha la Simba Day lililofanyika katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Simba ilipocheza na Asante Kotoko ya Ghana.

Video hiyo ilianza kusambaa tangu juzi jioni na kuwa maarufu kwa kupata wachangiaji wengi ndani na nje ya nchi waliokuwa wakilaani kitendo cha askari hao kumpiga mwandishi hadi kumvua nguo.

Video hiyo inaonyesha askari wakimpiga mwandishi huyo ingawa alitii amri na kukaa chini baada ya kuona wanaendelea kumshushia kipigo kikali.

Mjadala mkali uliibuka kwenye mitandao ya kijamii kuanzia WhatsApp, Facebook na Instagram huku wananchi wengi, katika michango yao, wakiwashutumu askari hao kwa kitendo hicho.

Fatma Karume, Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), alisema chama hicho kiko tayari kumpa msaada wa kisheria mwanahabari huyo anayedaiwa kushambuliwa na polisi.

Mshambuliaji wa timu ya taifa Tanzania na Klabu ya KR Genk, Mbwana Samatta, aliandika katika Twitter yake akisema: “Si kitendo cha kiungwana askari kupiga mwandishi katika eneo la michezo. Mpira ni mchezo unaoleta amani na si kuvunja Amani.”

Wachangiaji kwenye mitandao ya kijamii baadhi waliandika: “Hii haipaswi kukaliwa kimya, hata angekuwa mhalifu hapaswi kupigwa kiasi hicho.”

Mchangiaji mwingine aliandika: “Najiuliza shati lake liko wapi? Je, huyu ni mwizi, kibaka, alipigana, aliingia uwanjani wakati wanacheza? Vyote hapana. Alikuwa katika majukumu yake halafu anapigwa hivi. Kwa  hili viongozi wa Jeshi la Polisi tunaomba mchukue hatua kwa hawa askari. Sidhani kama mtu mpaka katii amri, kalala chini bado anapigwa, si sahihi inaumiza sana.”

Jana mchana, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa aliitisha mkutano na waandishi wa habari na kusema polisi inalaani kitendo hicho na tayari wameshaanza uchunguzi.

Alisema hakuna aliye juu ya sheria, awe mwandishi au askari wakikosea sheria itachukua mkondo wake.

“Tunafanya uchunguzi na uzuri wale askari walionekana kwa hiyo taratibu zikikamilika wahusika watachukuliwa hatua,” alisema.

“Polisi Kanda Maalum imeanza uchunguzi wa tukio hili kwa kufungua jalada la uchunguzi wa picha ya video hiyo inayosambaa inayoonyesha askari Polisi na mwandishi huyo wa habari ili kubaini ukweli,” alisema.

Alisema uchunguzi huo unakwenda sambamba kwa kumtaka mtendewa wa kosa hilo la kupigwa kutoa taarifa kituo cha Polisi ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa.

Kamanda Mambosasa alisema hadi alipokuwa anazungumza jana hakuna kituo chochote cha polisi chenye taarifa ya kupigwa kwa Mbise na kwamba ameshaagiza jalada la uchunguzi lifunguliwe na baadhi ya askari wameshahojiwa.

“Mtu yeyote anatakiwa kutoa malalamiko yake pale anapoona ametendewa vitendo ambavyo ni kinyume cha sheria hivyo Mbise akatoe taarifa kituo cha polisi,” alisema.

 “Polisi jukumu lake kuu ni kulinda usalama wa raia na mali zao na si kuwapiga raia walitenda kosa ambao hawajakataa kutii sheria ya kukamatwa, hivyo tunalaani tukio hili” alisema

MCT, TASWA WALAANI

Baraza la Habari Tanzania (MCT) na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (Taswa) kwa pamoja wameeleza kusikitishwa, kufedheheshwa na kukasirishwa na tukio la ukatili lililofanywa na polisi hao.

Katibu Mtendaji wa MCT, Kajubi Mukajanga, na Katibu Mkuu wa Taswa, Amir Mhando, jana walitoa taarifa ya pamoja ambayo ndani yake walieleza kuwa kwa mujibu wa Mbise tukio lilitokea baada ya mchezo wa Tamasha la “Simba Day”.

“Kama ulivyo utaratibu mchezo ukimalizika waandishi wa habari wanakwenda kuzungumza na makocha katika eneo maalum lililotengwa.

“Wakati akielekea eneo hilo baadhi ya askari walikuwa wakizuia waandishi kuingia eneo hilo na alipojaribu kuwaelewesha na kujitambulisha ndipo akafanyiwa ukatili huo wa kupigwa na kuumizwa,” lilieleza tamko hilo la pamoja.

Pia tamko hilo lilisema kuwa tukio hilo na mengineyo ya kikatili wanayofanyiwa wanahabari wakiwa kazini hayatafumbiwa macho kwani siyo udhalilishaji wa taaluma ya habari tu bali inachukuliwa kuwa ni hujuma kwa tasnia.

“Inachukuliwa kuwa ni hujuma kwa tasnia kwa nia ya kudhoofisha uhuru wa kupatikana kwa habari na usambazaji wa habari kwa jamii ikiwa ni nguzo kuu kwenye mfumo wa kidemokrasia, ambao tunajitahidi kuuimarisha nchini,”lilieleza tamko.

Kwa pamoja tamko hilo, lilikumbusha kuwa vyombo vya habari ni nguzo muhimu ya kujenga jamii yenye uelewa wa mambo mbalimbali yanayoendelea nchini kama inavyoainishwa kwenye Ibara ya 18 ya Katiba.

“Ikumbukwe, kitendo hicho ni kinyume na ibara ya 13(6) (e) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayokataza mtu kuteswa. Kukaa kimya hata tukiliwazwa na kuombwa samahani kwa jambo hili, hakutatoa tafsiri nyingine kwa wana taaluma ya habari na jamii kwa ujumla isipokuwa kuliona jambo hili kama ni la kawaida,”lilieleza tamko hilo.

Pia tamko hilo lilieleza kuwa waandishi wana kila haki ya kufanya kazi zao bila kusumbuliwa, kupigwa au kutishwa.

“Tunatarajia Jeshi la Polisi kufanya kazi zake kwa kufuata sheria na weledi wa kazi na kuwa walinzi wa amani na mali za wananchi. Mbise kwa hivi sasa yupo katika matibabu kutokana na kipigo hiki. Tunataka polisi wote waliohusika katika kitendo hiki cha kikatili wachukuliwe hatua kali ili wasiendelee kulipa taswira mbaya jeshi zima la polisi,” lilisema.

Tamko hilo lilikumbusha kuwa, kifungu cha 7 (1) cha Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari, 2016 inatoa haki na wajibu kwa vyombo vya habari kukusanya, kuchakata na kusambaza habari na taarifa mbalimbali kwa wananchi.

Pia tamko hilo lilieleza kuwa TASWA juzi ilifanya kikao na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuhusu jambo hilo.

 

 

Kadhalika, tamko hilo lilisema kuwa TASWA itaandaa kikao na wahariri wa habari za michezo kuona namna ya kujadili masuala ya usumbufu wa wanahabari viwanjani kabla ya Ligi Kuu Tanzania Bara haijaanza.

“Baraza la Habari, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania wanawasiliana na wanasheria wao kwa ajili ya kufungua mashtaka dhidi ya wahusika kwa vitendo vya mateso (tourture” alivyofanyiwa ndugu Mbise,” lilieleza.

Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF), nalo lilitoa taarifa jana likilaani tukio hilo.

“Tayari TFF imekutana na viongozi wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo (Taswa) na kujadiliana kuhusu tukio hilo na hatua stahiki,” ilisema taarifa hiyo.

Habari Kubwa