Polisi waua 3 kwa tuhuma kuua watu 6 kwa mapanga

24Sep 2018
Gurian Adolf
SUMBAWANGA
Nipashe
Polisi waua 3 kwa tuhuma kuua watu 6 kwa mapanga

POLISI wilayani Nkasi mkoani Rukwa wamewaua kwa kuwapiga risasi watu watatu wakati wakijaribu kutoroka wakiwa chini ya ulinzi.

Tukio hilo lilitokea Septemba 20 saa 5:00 usiku katika barabara ya Nkundi kuelekea kijiji cha Kate, Kata ya Kipande wilayani humo baada ya watu hao waliokuwa wakituhumiwa kufanya mauaji ya watu sita kwa kuwakata mapanga na mashoka, baada ya kuruka katika gari la polisi na kutaka kukimbia.

Kamanda wa polisi mkoani Rukwa, George Kyando, aliwataja waliouawa kwa kupigwa risasi na polisi ni Nching'wa Njige (44), Dashina Ngeseyamawe (46) ambao ni wakazi wa kijiji cha Ntalamila na Joseph Jiuke (34) mkazi wa kijiji cha Chonga.

Alisema kuwa watu hao walikuwa wamepakiwa kwenye gari la polisi ili waende kuwaonyesha polisi watuhumiwa wenzao ambao walikuwa wakitafutwa kwa kushiriki kufanya mauaji ya watu sita kwa kuwakata mapanga na shoka kutokana na imani za kishirikina.

Kamanda Kayando alisema kuwa waliokuwa wanatafutwa ni Mabula Sokoni, Said Tongela pamoja na mganga wa jadi, John Luchwela, ambaye aliwapa dawa ili wasikamatwe baada ya kufanya mauaji hayo.

Wakiwa wanaelekea kuwaonyesha watuhumiwa wengine, ndipo waliporuka katika gari la Polisi ili watoroke, kitendo kilichosababisha polisi kuwafyatulia risasi.

Watuhumiwa hao walikamatwa kufuatia msako ulioanza Julai 1 na walipohojiwa na polisi walikiri kufanya mauaji ya watu sita kwa kuwakata mapanga na mashoka.

Waliwataja waliowaua ni Naomi Ng'wanamayunga, mkazi wa kijiji cha Ntuchi Samweli Seki, Mkazi wa kijiji cha Ntalamila, Jibuta Majebele, mkazi wa kijiji cha Mkole, Odoviko Sumuni, mkazi wa kijiji cha Chonga, Salome Kisinza, mkazi wa kijiji cha Chalachima na Said Matenga, mkazi wa kijiji cha Mwai kwa madai kuwa ni wachawi.

Kamanda huyo alisema kabla ya kuuawa kwa kupigwa risasi na polisi, watuhumiwa hao katika mahojiano walikiri pia kuwaua watu zaidi ya 15 kwa nyakati tofauti katika mikoa ya Rukwa, Katavi na Simiyu.

Walikiri  watu sita kati ya 15 waliwaua katika wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa kwani wamekuwa wakikodiwa katika sehemu mbalimbali kwa ajili ya kufanya mauaji ya watu wanaodhaniwa kuwa ni wachawi.

Kamanda huyo alisema kuwa miili ya marehemu hao imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Mkoa ya Sumbawanga kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

Habari Kubwa