Polisi waua wawili madai ya ujambazi

20Oct 2020
Allan lsack
ARUSHA
Nipashe
Polisi waua wawili madai ya ujambazi

JESHI la Polisi Mkoa wa Arusha, limewaua watu wawili wanaotuhumiwa kuwa ni majambazi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Kamishna Msaidizi, Salum Hamduni.

Watuhumiwa wengine watatu wa ujambazi, wanadaiwa kukimbia wakati wa jeshi hilo likiendelea na shughuli ya upekuzi katika eneo la tukio, ilikopatikana silaha moja aina ya Shotgun ikiwa na risasi tisa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Kamishna Msaidizi, Salum Hamduni, alisema tukio hilo lilitokea Oktoba 18, mwaka huu, majira ya saa 1:30 mchana katika eneo la Olkerian Kata ya Moshono jijini Arusha.

Kamanda Hamduni, aliwataja watuhumiwa hao, wa ujambazi kuwa ni Bashiri Ally na mtuhumiwa mwingine alifahamika kwa jina moja la Mohamed.

Alisema kuwa baada ya watuhumiwa hao, kutaka kukimbia polisi walifyatua risasi juu kuwaonya wasikimbie badala yake waliendelee kukimbia na walianza kurushiana risasi na askari polisi, hali iliyosababisha Bashiri Ally, kujeruhiwa sehemu za miguu na mgongoni.

Alisema baada ya kurushiana risasi na askari polisi walijerujiwa na wakati wakipelekwa hospitalini kwa ajili ya kupatiwa matibabu walifariki dunia.

Hata hivyo, alisema kabla ya umauti Mohamed akiwa anapelekwa hosipitali alihojiwa na kuwataja watuhumiwa wengine watatu majambazi waliotoroka, pia walieleza kuwa walikuwa na silaha nyingine mbili aina ya bunduki (shotgun) na bastola waliziangusha katika eneo la tukio wakati wakirushiana risasi na askari polisi.

“Kwa kuwa siku hiyo, kulikuwa na giza upekuzi ulifanyika tena asubuhi ya Oktoba 18, kwa kushirikiana na wananchi tulifanikiwa kuzipata silaha mbili aina ya Bastola aina ya Bereta isiyokuwa na namba ikiwa na risasi nne ndani ya magazine,”alisema Hamduni.

Aidha, alisema jeshi hilo, linaendelea na msako ili kuwakamata watuhumiwa waliotoroka katika tukio hilo, pia jeshi la polisi limewaomba wananchi kutoa taarifa ili kufanikisha shughuli ya kuwakamata wahusika hao.

Habari Kubwa