Polisi yakuta bunduki 6 zilizotelekezwa

02Jul 2019
Gideon Mwakanosya
SONGEA
Nipashe
Polisi yakuta bunduki 6 zilizotelekezwa

SIKU chache baada ya Watanzania tisa kuuawa kikatili mpakani mwa Tanzania na Msumbiji na watu wanaosadikiwa kuwa ni magaidi, Jeshi la Polisi mkoani Ruvuma limeendesha msako na kukamata bunduki sita aina ya gobole zilizotelekezwa na watu wasiojulikana.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma, ACP Simon Marwa, alitoa taarifa hiyo wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini hapa kuhusu matukio mbalimbali ya kihalifu yaliyotokea mkoani humo.

Kamanda Marwa alisema kuwa kuanzia Juni 23 hadi 27, jeshi hilo liliendesha msako mkali na jumla ya bunduki sita zisizo na namba aina ya gobole zilizotengenezwa kienyeji zilikutwa zimetelekezwa katika maeneo mbalimbali zikiwa katika ofisi za vijiji vya Mpepo, Kihurunga na Liparamba vilivyopo katika kata ya Mpepo na Liparamba wilayani Nyasa mpakani mwa Tanzania na Msumbiji.

Kamanda alisema katika msako huo waliwatia mbaroni watuhumiwa kadhaa akiwamo Hassan Selemani (47), aliyekamatwa Juni 27 majira ya saa 7.00 usiku akiwa na meno manne ya tembo yenye uzito wa kilogramu 13.

Pia Juni 29, majira ya saa 10 usiku katika Kijiji cha Magazini, kata ya Lusewa wilayani Namtumbo mkoani hapa, Rashid Komba (33), alikamatwa akiwa na mkia wa tembo aliouhifadhi nyumbani kwake, wenye thamani ya Dola za Kimarekani 15,000 sawa na Sh. 34,465,000.

Vile vile, jeshi hilo lilimkamata Hadrack Marekela (22), kwa tuhuma za kuvunja na kuiba Tv nne na raia wa kigeni kutoka Sri Lanka, Hamid Sally Ishrath Ibrahim(47) na Segu Mohamed Ruwaisi (63), wamekamatwa wakiwa na madini aina ya Sulphire yenye uzito wa gramu 8.3 waliyoyanunua bila ya kufuata utaratibu na kuyaficha ndani ya nyumba yao.

Pia mtuhumiwa Mohamd Ismail (22), alikamatwa na polisi akiwa na mtambo wa kutengenezea pombe ya moshi.