Polisi yaomba msaada Interpol

05Jul 2019
Beatrice Moses
Dar es Salaam
Nipashe
Polisi yaomba msaada Interpol

JESHI la Polisi limesema linaunganisha nguvu  na Polisi Kenya kupitia Shirika la Kimataifa la Polisi (Interpol) kuchunguza tukio linalomhusu mfanyabiashara wa Kenya, Raphael Ongangi, aliyedaiwa kutekwa hivi karibuni.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, alisema wanachunguza mazingira ya kupatikana kwa Ongangi ambaye alidaiwa kutekwa nyara nchini Tanzania  wiki iliyopita na kupatikana juzi Mombasa, Kenya. Tukio hilo linahusishwa na mambo ya kisiasa.

“Nilizungumza na afande IGP  kuna maagizo amenipa tunayafanyia kazi. Tunaendelea kuwasiliana na wenzetu Interpol, tutawafikia wenzetu wa Kenya ili kujua mazingira yaani mtekaji akuteke Tanzania akuchukue hadi Mombasa,  ukutwe karibu na shangazi yako!" Alisema.

 "Hatuelewi chanzo cha habari hii maana taarifa zenyewe zilikuwa zinatia shaka, tunachunguza kama ni tukio la kutengeneza muhusika atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria," alisema.

Mambosasa alibainisha kuwa   taarifa zenyewe zilitolewa  kwa shaka kubwa hasa kwa kuwa mtoa taarifa pia aliwahi kutoa madai ya kutaka kutekwa.

"Mwaka juzi nilipokuwa kule Dodoma yeye mwenyewe aliwahi kuzua kuwa  yeye anataka kutekwa, lakini nilimwambia kuwa Jeshi la Polisi linafuatilia hilo. Hakuna  yeyote aliyesema  hayo labda kama anataka kujiteka ajiteke mwenyewe," alisema Mambosasa  bila kumtaja jina mtoa taarifa huyo.

Ongangi alidaiwa kutekwa akiwa na mkewe, Veronica Kundya, Jumatatu usiku katika maeneo ya Oysterbay jijini Dar es Salaam na watu wenye silaha ambao baadaye walimshusha mkewe na kuondoka naye.

Wakati huo huo, Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, wamewaua watu wawili wanaodaiwa kuwa  majambazi.

Hata hivyo, Kamanda Mambosasa alisema kuwa majina ya watu hao bado hayajafahamika.

Alisema Julai Mosi, mwaka huu,  majira ya saa 8:30 mchana katika maeneo ya Kitunda Machimbo, kikosi kazi maalum cha kuzuia na kupambana na majambazi kikiwa maeneo hayo kwa ajili ya kufuatilia majambazi sugu, kilikutana uso kwa uso na watu wawili ambao walianza kuwarushia risasi baada ya kubaini kuwa wamezingirwa na askari.

Mambosasa alisema baada ya mapambano hayo, majambazi hao walijeruhiwa na kupelekwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na baada ya  daktari kuwachunguza, alithibitisha wamefariki dunia na miili ya marehemu imehifadhiwa hospitalini hapo.

Alibainisha kuwa polisi walipata silaha walizokuwa wakitumia majambazi hao ambazo ni bastola mbili aina ya Browning yenye namba A.558816 ikiwa na risasi tatu ndani ya magazine na nyingine yenye namba A.963815 TZCAR 101418 ikiwa na risasi mbili.

Habari Kubwa