Polisi yaonya wagombea, wafuasi

30Sep 2020
Augusta Njoji
Dodoma
Nipashe
Polisi yaonya wagombea, wafuasi

​​​​​​​JESHI la Polisi limetoa tamko kwa wagombea na wafuasi wao likiwataka kuacha kutoa lugha za matusi na kupandikiza chuki kwa wananchi

Kamishna wa Operesheni na Mafunzo, Liberatus Sabas.

Pia, limewataka kufuata ratiba ya kampeni iliyotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), huku likisema halitamuonea aibu mtu yeyote atakayekwenda kinyume cha sheria za nchi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamishna wa Operesheni na Mafunzo, Liberatus Sabas, baadhi ya wagombea  wamekuwa wakitoa lugha za matusi, uzushi na uongo, kashfa kwa wagombea wengine jambo ambalo ni kinyume na maadili na taratibu za uchaguzi.

Alikemea tabia ya wafuasi kuchana bendera na mabango ya wagombea wengine.

“Miongoni mwa matatizo yanayojitokeza ni pamoja na baadhi ya wagombea kutofuata ratiba ya kampeni iliyotolewa na Tume,” alisema.

Alisema vyama vyote vinatakiwa kufuata ratiba na kama kuna chama kinataka kubadili ratiba kinatakiwa kuwasiliana na Mkurugenzi wa NEC.

“Kuna mgombea mmoja anafanya kwa makusudi kwenda kufanya mikutano sehemu ambayo hana ratiba ya kampeni, umuhimu wa kufuata ratiba ni kulifanya jeshi kutoa ulinzi kwenye hiyo mikutano, kwenda sehemu ambazo hayupo kwenye ratiba ni kujipeleka hatarini,” alisema.

Alisema jeshi hilo lipo kwa ajili ya kuhakikisha kila mmoja anakuwa salama na kusisitiza kuwa watasimamia ratiba ya NEC na mgombea atafanya mkutano sehemu aliyoelekezwa.

“Tuliacha haya mambo yakawa yanaenda kienyeji kuanzia sasa tutaanza kuchukua hatua, maana tusipochukua hatua likitokea la kutokea sisi Jeshi la polisi ndio tutakaolaumiwa kwamba hatukutoa ulinzi ndio maana watu hawa wamezulika,” alisema.

Kadhalika, alisema kuna wagombea baada ya kumaliza kampeni zao wanaamua kuingia mtaani kwa maandamano hadi usiku wakati ratiba inasomeka mwisho saa 12 jioni.

“Huko mtaani usiku usalama wako utakuwa hatarini na wakipata matatizo watakuja kulaumu Jeshi la Polisi, sasa nasema chama chochote chenye kampeni inapofika muda wa kumaliza kampeni watawanyike warudi nyumbani kwao, atakayekwenda kinyume na hapo tutachukua hatua,” alisema.

“Kuna watu wanatoa vitisho kwa viongozi wa polisi na serikali, kila nchi inaongozwa kwa misingi ya kisheria, kanuni na taratibu zake, ambaye hatafuata tutamchukulia hatua bila kujali hayo anayosema,” alisema Sabas.

Aliwataka wananchi kutokubali kudanganywa kujiingiza kwenye vurugu na kuzipa tabu familia zao huku viongozi wao wakitanua mtaani.

“Jeshi la polisi lisingependa kutumia silaha wakati fedha zao ndio zimenunua, sisi ni sehemu ya familia tusingependa kupambana na wananchi ambao sisi ni sehemu yao, wananchi watii sheria bila shuruti ili nchi imalize uchaguzi kwa amani na utulivu,”alisema.

Habari Kubwa