Polisi yaua 3 Dar wakidai majambazi

06Dec 2017
Romana Mallya
Nipashe
Polisi yaua 3 Dar wakidai majambazi

JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, limewaua watu watatu wanaodaiwa kuwa ni majambazi, akiwamo raia ya Burundi.

Kamanda wa kanda hiyo, Lazaro Mambosasa, alisema jana, mwishoni mwa mwezi uliopita askari walifanya oparesheni maalum na kuwakamata watu watatu wanaotuhumiwa kujihusisha na matukio ya uporaji na mauaji jiji  Dar es Salaam. 

Alisema baada ya mahojiano watuhumiwa walikubali kuonyesha bunduki moja aina ya AK.47, magazine mbili na risasi 57 ambayo walikuwa wameificha kwenye kichaka karibu na eneo la Ubungo Mawasiliano.

Pia alisema watu hao walionyesha  pikipiki mbili aina ya Boxer zenye namba za usajili MC 757 BCT rangi nyekundu na MC 946 BSE rangi nyeusi ambazo walizipora katika matukio mbalimbali. 

“Katika mahojiano walikiri kuwa na silaha nyingine ambazo wamezificha kwenye kichaka eneo la Ununio na wako tayari kwenda kuonyesha silaha hizo, walipofika huko wakati wakishuka kwenye gari mmoja wao raia wa Burundi, Fanuel Kamana maarufu Mrundi, alimvamia askari kwa lengo la kumpora silaha,” alisema na kuongeza:

Wakati huyu akijaribu kupora silaha, wenzake wawili ambao ni Gallus Clement (31) na Fredrick Acholo, nao walitaka kutoroka, hivyo polisi waliwajeruhi kwa risasi na wote walifariki njiani wakipelekwa Mwananyama hospitali ambapo miili yao imehifadhiwa.”

Pia alisema majambazi hao walikiri kufanya matukio kadhaa ya uporaji na mauaji, likiwamo tukio la mauaji huko Kunduchi Mtongani lililotokea Novemba 19, mwaka huu ambapo huwaua madereva bodaboda na kupora pikipiki zao na kuziuza kwa Sh. 800, 000,” alisema.

Katika hatua nyingine, Mambosasa alisema eneo la Mbezi Msumi wamekamata gari T 142 CNF rangi ya “silver”, redio call aina ya Motorola, kamba za katani na vipande viwili vya nondo vilivyokuwa vikitumiwa na kundi la majambazi watano.

Alisema watu hao walikwenda nyumbani kwa Erick Mkwemwa na kujitambulisha kuwa ni maofisa wa Polisi waliofika hapo kwa ajili ya kufanya upekuzi, lakini badala yake waliwaweka chini ya ulinzi familia hiyo na kuwafunga kamba mikononi, miguuni kisha kuwaziba na plasta mdomoni.

Alisema majirani wa eneo hilo walitilia shaka kitendo hicho na kuamua kuizingira nyumba hiyo huku wakitoa upepo matairi ya gari.

Wakati huo huo, Kamanda Mambosasa alisema limekamata Bastola ambayo imetengenezwa kienyeji (bastola feki) iliyokuwa inatumiwa na jambazi sugu katika matukio ya uporaji wa pikipiki maeneo ya Buza Sigara.

Alisema jambazi aliyekutwa na bastola hiyo alimkodi dereva pikipiki ili ampeleke maeneo ya Msitu wa Jeshi huko Buza lakini ghafla walipofika maeneo hayo mtu huyo alitoa bastola yake iliyotengenezwa kienyeji ikiwa na baruti.

Alisema jambazi huyo alimuamuru dereva ashuke na kumuachia pikipiki, baada ya kushuka dereva alipiga kelele kuomba msaada na ndipo wananchi walijitokeza na kuanza kumpiga kwa mawe huku wengine wakimkata mapanga. Alisema polisi walipofika eneo la tukio walimkuta akiwa amejeruhiwa na alifariki njiani akipelekwa hospitali ya Temeke.

 

Habari Kubwa