Polisi yazuia mkutano wa ndani wa Chadema

22Jan 2020
Marco Maduhu
Shinyanga
Nipashe
Polisi yazuia mkutano wa ndani wa Chadema

JESHI la Polisi mkoani Shinyanga limeuzuia mkutano wa ndani wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), baada ya kutokea sintofahamu kati ya viongozi wa chama hicho kikuu cha upinzani nchini.

Hatua hiyo ilichukuliwa kufuatia kitendo cha Katibu Mwenezi wa chama hicho Jimbo la Shinyanga, Charles Shigino, kuandika barua kwa Jeshi hilo akidai kutoufahamu.

Kadhalika, Shigino alidai kwenye barua hiyo kuwa mkutano huo unahatarisha hali ya usalama.

Akizungumzia kuzuiwa mkutano huo, Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Shinyanga, Emmanuel Ntobi, alisema walitarajia kufanya mkutano huo kwa ajili ya kupeana maelekezo ya chama kutoka ngazi za juu sambamba na mikakati ya kukijenga chama kuelekea kwenye uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.

Alisema wakati akijiandaa na mkutano, walikuta askari Polisi wakiwa wametanda kwenye eneo ambalo walipanga kuufanyia katika Hoteli ya Ibanza Kata ya Ibinzamata Mjini Shinyanga, na kuambiwa hawawezi kuufanya kutokana na taarifa walizopewa za hali ya kiusalama.

“Wakati tukijiandaa na mkutano huo ndipo Jeshi la Polisi likatuzuia kutoufanya na tulipohoji ni kwanini, tukaambiwa kuwa Katibu Mwenezi wetu ameandika barua Polisi ya kutoutambua mkutano, na kwamba una hatarisha hali ya usalama, ndipo kuamua kuuhairisha hadi siku nyingine,” aliongeza Ntobi.

Alisema kutokana na katibu mwenezi huyo kukiuka katiba ya chama na kuonyesha utovu wa nidhamu pamoja na kukisaliti chama, Baraza la Uongozi la Mkoa limeadhimia kumsimamisha nafasi zake za uenezi Jimbo la Shinyanga na ujumbe wa Mkutano Mkuu Kata ya Ngokolo.

Shigino, alikiri kuandika barua kwa Jeshila Polisi kuzuia mkutano huo kwa madai ni batili na umekiuka katiba ya chama, akidai hakupewa taarifa juu ya kuwapo kwa mkutano huo wakati yeye ndiye mratibu wa mikutano yote, ndipo akaamua kuuzuia.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga, Deborah Magiligimba, alithibitisha kuuzuia mkutano, baada ya kutokea kutokuelewana kati ya viongozi wa chama hicho kwa kuwa ni hatari kiusalama.

Alisema Jeshi hilo liliwapa sharti la kuelewana kwanza ndipo waruhusiwe kufanya mkutano huo tena.

Habari Kubwa