PPRA yaokoa fedha za serikali bil. 46/-

17Jul 2019
Beatrice Shayo
Dar es Salaam
Nipashe
PPRA yaokoa fedha za serikali bil. 46/-

MAMLAKA ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) imeisaidia serikali kuokoa Sh. bilioni 46.91 ambazo zingepotea kutokana na kutokufuatwa kwa taratibu za ununuzi na usimamizi wa mikataba.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa PPRA, Mhandisi Leonard Kapongo.

Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Ofisa Mtendaji Mkuu wa PPRA, Mhandisi Leonard Kapongo, wakati wa kongamano la saba la Usimamizi wa Manunuzi ya Umma.

Alisema fedha hizo zimeokolewa katika kipindi cha mwaka 2016/17 hadi 2017/18, zilibainika wakati PPRA ikifanya uchunguzi maalum ili kubaini ukiukwaji wa taratibu za manunuzi.

Kapongo alisema fedha zilizookolewa ni malipo ya makandarasi na watoa huduma kinyume na utaratibu na hivyo taasisi hizo zikaelekezwa kurejesha fedha hizo.

Vile vile, alisema PPRA inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwamo baadhi ya taasisi kutotoa ushirikiano  wakati wa ukaguzi.

Alisema baadhi ya taasisi kutowasilisha PPRA ripoti na taarifa mbalimbali za zabuni kwa wakati hivyo kuikwamisha mamlaka katika utekekeza majukumu yake.

"Baadhi ya taasisi za serikali kutokusimamia ipasavyo utekelezaji wa mikataba ya manunuzi na kukwamisha upatikanaji wa thamani bora ya fedha," alisema.

Kapongo alisema kuna changamoto ya uhaba wa watumishi wenye taaluma ya manunuzi katika taasisi zinazoshughulikia masuala ya manunuzi ya umma, kuanzia ngazi ya usimamizi hadi utekelezaji na kuathiri utendaji wa taasisi husika.

"Ufanisi mdogo kwa baadhi ya taasisi za serikali katika kuendesha michakato ya zabuni, hivyo kusababisha ongeleko la gharama na muda katika utekelezaji wa miradi," alisema Kapongo.

Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo, aliagiza yeyote aliyehusika na upotevu wa fedha za serikali kuchukuliwa hatua kali ikiwa ni pamoja na kurejesha fedha za serikali.

"Nilivyosikia kuna fedha za serikali takribani bilioni 46.9 zimeokolewa na chunguzi zilizifanywa na PPRA katika taasisi za umma katika miaka miwili tu kwa kukagua taasisi chache, naagiza waliohusika na upotevu wa fedha za serikali kuchukuliwa hatua kali," alisema.

Jafo alisema bodi za wakurugenzi na maofisa masuhuli wa taasisi za serikali wanahusika moja kwa moja katika kuhakikisha sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa katika manunuzi ya umma zinafuatwa kwenye taasisi.

Alisema uadilifu ndiyo msingi mkubwa wa uzalendo na huwezi kuwa tishio iwapo uwazi na iwajibikaji utakosekana katika manunuzi ya umma.

"Manunuzi yanaweza kutoa mwanya kwa watendaji wa sekta ya umma na binafsi kutumia fedha za umma kujinufaisha binafsi. Manunuzi ni sehemu kubwa ya shughuli za kiuchumi na hivyo huvutia sana vitendo vya rushwa na udanganyifu jambo ambalo lina athari kubwa kwa fedha za walipa kodi," alisema Jafo.

Awali Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya PPRA,  Prof. Sufian Bukurura, alisema wana uhaba wa rasilimali watu hivyo kuathiri utekelezaji wa majukumu kwani waliopo ni 74 ikilinganishwa na mahitaji ya wafanyakazi 152.

Alisema wanaiomba serikali iwaongezee watumishi kulingana na mahitaji kwa kuwa upungufu huo unaifanya PPRA isiweze kutekeleza majukumu yake kikamilifu kama vile kukagua taasisi nunuzi za kutosha kila mwaka.

Prof. Bukurura alisema ufinyu wa bajeti ambao unaifanya PPRA ishindwe kutekeleza majukumu yake kikamilifu hususani kwenye eneo la ukaguzi na kila mwaka PPRA hufanya kaguzi kwa wastani wa taasisi 100 tu kati ya taasisi zaidi ya 500 zilizopo.