Prof. Mkumbo ataka mamlaka za maji kutenga siku kusikikiza kero

15Jun 2019
Frank Monyo
Nipashe
Prof. Mkumbo ataka mamlaka za maji kutenga siku kusikikiza kero

Katibu Mkuu Mkuu Wizara ya Maji, Profesa Kitila Mkumbo ameagiza mamlaka za maji nchini kutenga siku maalumu ya kusikikiza kero za wananchi na kutoa mrejesho wa miradi ya maji inayoendelea.

Katibu mkuu Wizara ya maji profesa Kitila Mkumbo akizungumza na wananchi pamoja na wafanyakazi wa Dawasa.

Kauli hiyo ameitoa leo Juni 15,2019 wakati akizungumza na wananchi pamoja na wafanyakazi wa Dawasa katika ofisi zake zilizopo Kimara Matangini.

Amesema kwa sasa Dar es salaam usambazaji wa maji umefikia asilimia 85 hivyo mamlaka husika inapaswa kuhakikisha wananchi ambao hawajaunganishwa na mfumo wa maji ya DAWASA wanaunganishwa.

" Kwa sasa usambazaji wa maji kwa jiji la Dar es salaam ni asilimia 85 hivyo Dawasa wahakikishe wanawafikia watu ambao hawajaunganishwa na maji ya DAWASA ili kuhakikisha huduma ya maji inawafikia watu kwa asilimia 100," Amesema Profesa Mkumbo

Naye Meneja wa Dawasa wa Mkoa wa Ubungo Pascal Fumbuka, amesema kwa sehemu ambazo zina changamoto ya upatikanaji wa maji yana milima na mabonde hivyo kwa wakati mwengine maji yanakuwa na presha ndogo kuwafikia wananchi.

Amesema kuwa kwa sasa Dawasa Ubungo inahudumia wateja zaidi ya elfu 47 huku maeneo ya Kimara na Ubungo wanapata maji kwa asilimia 100, Kiluvya asilimia 90. " Changanyikeni asilimia 88, Msigani asilimia 62.

Amesema sehemu ambazo miundombinu ya maji imefika lakini maji hayajaanza kutoka ambayo ni King'azi A,B, Msumi, Mbezi Luisi, Msakuzi, Kisopwa, Njeteni na Marambamawili.

Nao wananchi walioudhuria katika kikao hicho wameipongeza DAWASA kwa kazi nzuri wanayofanya ikiwamo kutoa huduma nzuri kwa wateja.

"Mh mimi nawapongeza sana kwa kazi nzuri mnayofanya kama kwangu mimi maji napata na bili nalipa vizuri pia nawapongeza wafanyakazi wa Dawasa Kimara wanahudumia wateja vizuri ukifika hapa unahudumiwa vizuri kwa haraka," Amesema Asha Ramadhan

Habari Kubwa