Prof. Mkumbo ataka wahitimu CBE waache tabia ya kutafuta ajira

14Nov 2021
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe Jumapili
Prof. Mkumbo ataka wahitimu CBE waache tabia ya kutafuta ajira

WAHITIMU wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), wametakiwa kuacha tabia ya kuhangaika kutafuta ajira mara baada ya kuhitimu chuo na badala yake watumie elimu waliyoipata kutengeneza nafasi za ajira.

Waziri wa Viwanda na Biashara, Profesa Kitila Mkumbo, akizungumza kwenye mahafali ya 56 ya Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam ambapo wahitimu 800 walitunukiwa shahada kwenye fani mbalimbali.

Ushauri huo ulitolewa na Waziri wa Viwanda na Biashara, Prof.  Kitila Mkumbo, wakati wa mahafali ya 56 ya chuo hicho yaliyofanyika mwishoni mwa wiki chuoni hapo ambapo wahitimu 800 walitunukiwa shahada za fani mbalimbali.

Alisema wanaohitimu kwa mwaka mzima wanafikia 800,000 hivyo ajira haziwezi kutosheleza wahitimu wote na suluhisho pekee ni kwao kutafuta cha kufanya kwa kutumia elimu waliyoipata chuoni hapo.

“Nafasi za ajira serikalini ni chache mno na mnaohitimu kwa mwaka mzima ni kama laki nane sasa cha msingi mkihitimu leo hii msianze kutafuta ajira tafuteni kazi, kazi zipo ila ajira ndiyo hazipatikani. Kazi ni kile kitu ambacho wewe mhitimu unataka kufanya ambacho kitakuingizia kipato bila kuajiriwa popote,” alisema Prof Mkumbo.

 Vile vile, Prof Mkumbo alisema serikali inatambua na kupongeza mafanikio ya chuo hicho lakini inatambua changamoto za miundombinu ambazo chuo hicho bado kinakabiliana nazo.

Waziri wa Viwanda na Biashara, Profesa Kitila Mkumbo, akimpa cheti mmoja wa wanafunzi bora wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), kwenye mahafali ya 57 ya Chuo hicho yaliyofanyika chuoni hapo mwishoni mwa wiki.

Aliutaka uongozi wa chuo hicho kuweka msisitizo katika mafunzo ya biashara kwa wanachuo na kutoa mafunzo ya muda mfupi kwa wasiokuwa wanachuo na kufanya tafiti zinazolenga kutafua changamoto na matatizo katika sekta ya biashara na kutoa ushauri wa kitaalamu.

Alisema serikali inatambua umuhimu wa elimu ya biashara katika maendeleo ya nchi pamoja na kwamba nchi zinazokua kiuchumi kwa kasi kubwa kama Brazil, Urusi,, India, China na Afrika ya Kusini zimewekeza sana katika teknolojia na kuipa umuhimu elimu ya biashara.

Waziri wa Viwanda na Biashara, Profesa Kitila Mkumbo, na viongozi wa CBE wakiwa wamesimama kwa ajili ya wimbo wa Taifa kwenye mahafali ya 57 ya Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), mwishoni  mwa wiki jijini Dar es Salaam ambapo wahitimu 800 walitunukiwa shahada kwenye fani mbalimbali.

Alisema elimu ya ujasiriamali inahitaji wanachuo kuwa wabunifu na kushirikiana na watu wengine ili kuweza kufikia malengo waliyojiwekea.

Alisema nchini Tanzania elimu ya ujasirimali inahitajika sana ili kuzitumia kwa ufanisi fursa na rasilimali zilizopo kama vile maziwa, mito, bahari, mabwawa, madini, vivutio vya utalii na mazao ya misitu.

Kwa upande wake, Mkuu wa chuo hicho, Prof Emanuel Mjema alisema pamoja na kuongeza kozi chuo kimeendelea kujiimarisha katika suala zima la udhamini wa wahadhiri katika masomo ya shahada za uzamivu .

Makamu Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE),  akizungumza kwenye mahafali ya 56 ya chuo hicho yaliyofanyika mwishoni  mwa wiki jijini Dar es Salaam ambapo wahitimu 800 walitunukiwa shahada kwenye fani mbalimbali.

Alisema hilo linafanyika ili kuhakikisha chuo kinatoa elimu bora kulingana na uhitaji wa soko  na kwamba mpaka sasa chuo kimeendelea kuwasomesha wanataaluma wake kufikia kiwango cha shahada za uzamivu (PhD) kwa kutumia fedha za ndani.

Prof Mjema alisema kwa sasa chuo kina wanataaluma wahadhiri 35 wenye shahada za uzamivu  kati ya wahadhiri 192 na bado chuo kinafanya mipango mbalimbali kuhakikisha kinawaendeleza wahadhiri ambapo kwa sasa kinawasomesha wahadhiri 43 ngazi ya uzamivu na wahadhiri wengine 11 katika ngazi ya uzamili.

Aliiomba serikali iendelee kuwapa ufadhili wahadhiri wa chuo hicho ili waweze kujiendeleza kitaaluma katika ngazi za ashahada za Uzamivu ambazo ni muhimu kwa taasisi ya elimu ya juu.

Aliongeza kuwa chuo bado kina uhaba wa fedha za kufanya tafiti lakini aliishukuru serikali kwa kuendelea kuwalipa mishahara wafanyakazi wote wa chuo hicho.

“Huu ni mchango mkubwa sana kwa CBE ambao unahakikisha kuwa chuo hiki kama taasisi inajiendesha vizuri na kazi kubwa kwetu hapa ni kufundisha, kufanya tafiti na kutoa ushauri wa kitaalamu na jukumu la kufundisha linafanyika vizuri,” alisema

Wahitimu wa fani mbalimbali wakiwa kwenye mahafali hayo ya 56 yaliyofanyika mwishoni mwa wiki chuoni hapo.

Habari Kubwa