Prof Mkumbo atoa neno Dawasco

02Aug 2017
Na Mwandishi Wetu
Dar es salaam
Nipashe
Prof Mkumbo atoa neno Dawasco

Katibu Mkuu wa wizara ya Maji na Umwagiliaji, Profesa Kitila Mkumbo amesema ameapa kuwashughulikia watumishi wachache chini ya wizara yake ambao bado wanaendekeza maisha ya ujanja ujanja kazini.

Katibu Mkuu wa wizara ya Maji na Umwagiliaji, Profesa Kitila Mkumbo katikati, na Afisa Mtendaji Mkuu wa Dawasco Mhandisi Cyprian Luhemeja wakiwa na watendaji wengine wakiimba wimbo wa taifa.

Profesa Kitila ameitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza na watendaji na mameneja wa Shirika la Maji Safi na Taka Dar es Salaam (Dawasco) kwenye ofisi za makao makuu ya shirika hilo jijini Dar es Salaam.

Amesema ingawa Dawasco imefanikiwa kuboresha huduma zake, lakini wapo watumishi wa chache ambao bado wanafanya kazi kwa ubabaishaji.

Amesisitiza kuwa zama za ujanjaujanja zimekwisha na wale wachache wanaoshiriki mbinu za kulihujumu shirika hilo hawatavumiliwa na watendaji wa shirika hilo kutoa taarifa kwa watakaobainika.

Alisema kuwa siku hizi simu za malalamiko anazopigiwa na wateja kuhusu huduma za maji zinazotolewa na Shirika hilo zimepungua. na badala yake anapokea ujumbe mfupi wa kupongezwa kuhusu huduma za zinatolewa na Dawasco.

"Nataka muundelee na kuchapa kazi kwa kutoa huduma bora kwa wakazi wa mikoa ya Dar es Salaam na Pwani kwani nyie ndiyo taswira ya Serikali katika utoaji wa huduma za maji, bila nyie ukatibu wa Mkuu hauna maana kwa Mkoa wa Dar es Salaam hata Waziri na wizara kwa ujumla,” alisema Mkumbo.

Habari Kubwa