Prof. Ndalichako ataka EP4R kuendelea kutoa fedha ujenzi shule

24Oct 2019
Kelvin Innocent
Dar es Salaam
Nipashe
Prof. Ndalichako ataka EP4R kuendelea kutoa fedha ujenzi shule

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof Joyce Ndalichako, ameutaka mradi wa EP4R uendelee kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu katika shule zote za serikali huku lengo kubwa likiwa ni kuwaandalia wanafunzi mazingira bora ya kujisomea. 

Ndalichako amesema hayo leo baada ya kutembelea shule ya sekondari Jikomboe iliyopo wilayani Chato mkoani Geita, huku akionyesha kuridhishwa na ujenzi unaoendelea katika shule hiyo.

Amesema uboreshaji wa miundombinu mashuleni ni suala endelevu ambalo limelenga zaidi kuhakikisha wanafunzi wote wanakuwa katika mazingira mazuri yatakayowapelekea kusoma kwa werevu zaidi. 

“Mpaka sasa katika mradi huu wa EP4R tumeshatumia  bilioni 306 kwa ujenzi wa madarasa karibia nchi nzima, na malengo yetu ni kutoa nafasi nyingi zaidi kielimu wa watu wote huku tukiamini ufaulu utaongezeka kutokana na mazingira ya shule kuwa rafiki pamoja na  kutatua changamoto mbalimbali mashuleni hasa zile shule zinazofanya vizuri tutazipa kipaumbele zaidi” Amesema Ndalichako.

Aidha, Ndalichako amesema serikali haiwezi kupeleka fedha popote kabla ya kubaini tatizo lililopo, pia ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Chato kwa kusimamia vizuri miradi ya ujenzi mashuleni.

 “Hatuwezi kupeleka fedha kabla ya kubaini tatizo ni nini na kulichukulia hatua,  Lakini napenda kuishukuru halmashauri ya Wilaya ya Chato mnafanya vizuri katika usimamizi wa ujenzi hivyo hatuna  sababu yeyote ya serikali kutoendelea kuwekeza katika miundombinu ya sekta ya elimu.” Amesema.

Habari Kubwa