Prof. Shemdoe awaonya matapeli ajira 6,000 za walimu

23Apr 2021
Na Mwandishi Wetu
DODOMA
Nipashe
Prof. Shemdoe awaonya matapeli ajira 6,000 za walimu

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais - TAMISEMI, Prof.Riziki Shemdoe, ametoa onyo kwa watu wanaowatapeli wananchi sehemu mbalimbali kwamba wanahusika kwa namna moja ama nyingine katika zoezi la kuajiri walimu 6,000 ili kujaza nafasi zilizoachwa wazi, kama ilivyoagizwa na Rais Samia Suluhu Hassan hivi karibuni.

Mwalimu akiwa darasani. picha na mtandao.

Ametoa onyo hilo leo Aprili 23, 2021 mbele ya waandishi wa habari wakati wa ziara yake ya kwanza Makao Makuu ya Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) Dodoma, iliyolenga kujionea utekelezaji wa majukumu yao pamoja na kuzungumza na watumishi.

Prof. Shemdoe amewataka watumishi wa umma kuepuka kujihusisha na utapeli huo kwani wakibainika watachukuliwa hatua kali za kinidhamu na kisheria ikiwemo kufukuzwa kazi. Aidha, kuhusu vishoka wanaojihusisha na utapeli huo, Prof. Shemdoe amesisitiza kuwa TAMISEMI itapambana nao vikali.

“Mtumishi atakayebainika kujiingiza kwenye suala hili la utapeli anaweza kupoteza kazi. Kwa wale vishoka ambao wameamua kujichukulia fedha za watanzania wenzetu wakiwahadaa kuwa watawatafutia ajira, tutapambana nao vikali na tutahakikisha sheria inachukua mkondo wake.”

Kufuatia hali hiyo, Prof Shemdoe amebainisha kuwa ajira husika zitatolewa kwa kuzingatia vigezo vitakavyoainishwa katika tangazo litakalotolewa na Ofisi yake, na kwamba hakutakuwa na upendeleo wa aina yoyote.

Habari Kubwa