Prof Shemdoe: Tutahitaji barua za wazazi uchaguzi wa tahsusi

06Jun 2021
Abdallah Khamis
Mtwara
Nipashe Jumapili
Prof Shemdoe: Tutahitaji barua za wazazi uchaguzi wa tahsusi

KATIBU Mkuu Ofisi ya Rais Tamisemi, Profesa Riziki Shemdoe, amesema Wizara yake inafikiria kuja na mpango wa kuwataka wazazi wenye watoto wanaotarajia kumaliza kidato cha nne kuandika barua maalumu ya michepuo wanayopendekeza watoto wao wajaze kwa ajili ya kuondoa mkanganyiko baina ya wanafunzi na w

Amesema baada ya taarifa kusambaa mitandaoni juu ya baadhi ya wanafunzi kuchaguliwa katika michepuo wasiyochagua, Wizara yake ilifuatilia na kugundua kuwa hali hiyo imetokana na kutokuwapo kwa mawasiliano sahihi baina ya mzazi na mwanafunzi juu ya michepuo waliyochagua.

Profesa Shemdoe ametoa kauli hiyo leo mkoani Mtwara wakati akizungumza na waandishi wa habari na kueleza kuwa hakuna mwanafunzi aliyepelekwa katika mchepuo asiouchagua kama taarifa hizo za mitandaoni inavyoeleza.

Alisema uchaguzi wa wanafunzi juu ya michepuo ulizingatia kuanzia chaguo la kwanza hadi la tano lililojazwa na mwanafunzi katika fomu maalum, pamoja na namna mwanafunzi alivyofaulu katika mchepuo husika.

“Hakuna ambaye amepangiwa asipochagua lakini tulichobaini ni mawasiliano duni baina ya wanafunzi na wazazi, kwamba mzazi anataka mwanae asome mchepuo huu na mtoto amejaza mchepuo mwingine sasa matokeo yanapokuja tofauti na waliyoongea mzazi ndiyo anaona mwanae ameonewa” amesema Profesa Shemdoe.

Amesema mfumo wa uchaguzi wa wanafunzi, juu ya tahsusi  ni wa kielektroniki, unaofanya uchaguzi na utambuzi na hupanga kulingana na ufaulu wa wanafunzi, hali inayoondoa uwezekano wa mwanafunzi kupangiwa tofauti na michepuo aliyoomba.

Ameongeza kuwa katika mfumo huo uchaguzi unaanza kwanza na yule aliyepata alama zote za A katika chaguo la kwanza na kama hajakidhi katika hatua hiyo sifa yake huhamishiwa katika hatua ya pili na kuendelea na pale atakapokidhi ndipo atakapopangiwa.

Aidha, alisisitiza  kuwa milango ya Tamisemi ipo wazi kwa wale wote  wanaoona hawajatendewa haki kwa ajili ya kuhakiki nafasi walizopangiwa watoto wao kutokana na tahsusi walizoomba.

Pia amebainisha kuwa baadhi ya wanafunzi wamepelekwa katika vyuo baada ya kukosa sifa katika tahsusi zote tano walizoomba huku wakiwa hawajajaza nafasi za vyuo.

“Wengine tuliona katika tahsusi zote tano walizoomba hawakuwa na sifa lakini huyu amefanya vizuri kwenye Chemistri na baiolojia sisi kama serikali tukaona huyu tusimuache mtaani tumpeleke katika vyuo vya afya lengo ni kumsaidia huyu” amesema Profesa Shemdoe.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Tamisemi anayeshughulikia elimu Profesa Gerald Mweri, amesema baadhi ya watu waliolalamika mitandaoni walipopigiwa simu kwa ajili ya kutoa ushirikiano juu ya madai ya wanafunzi kupangiwa wasipochagua hawakurejea tena kutoa ushirikiano

Habari Kubwa