Profesa Kanywanyi aagwa, azikwa Dar

13Jan 2021
Christina Mwakangale
Dar es Salaam
Nipashe
Profesa Kanywanyi aagwa, azikwa Dar

WAZIRI Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba, jana, aliongoza umati uliokusanyika kuuaga mwili wa mwanasheria nguli nchini na mkongwe wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Prof. Josephat Kanywanyi (82), aliyefariki dunia Jumapili.

Tukio hilo lililofanyika jana asubuhi kwenye ukumbi wa Nkrumah wa UDSM, lilikusanya umati wa wasomi na wanasheria, wakiwamo mawaziri na majaji.

Miongoni mwa mawaziri waliohudhuria ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba Kabudi, Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Mwigulu Nchemba, aliyeambatana na Jaji Mkuu, Prof. Ibrahim Juma.

Waziri Kabudi, ambaye miaka michache iliyopita, alikuwa mwanazuoni wa UDSM, aliwasilisha salamu maalum za majonzi kutoka kwa Rais John Magufuli.

Hadhira hiyo ambayo maziko yake yalifanyika katika makaburi ya Kinondoni, pia iliwakusanya Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, na wakongwe wa sheria UDSM, ambao sasa ni wastaafu akiwamo Prof. Issa Shivji na Dk. Ringo Tenga.

Ibada ya maziko ya msomi huyo ambaye pia amewafundisha wanasheria wengi nchini na nje ya nchi katika miaka yake 50 ya utumishi UDSM, iliongozwa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Kanisa Katoliki Dar es Salaam, Thaddaeus Ruwa’ichi.

Askofu Ruwa’ichi alimsifu Prof. Kanywanyi kwa mchango wake mkubwa nchini katika fani ya sheria na maboresho mbalimbali, sambamba na kanuni zake, akitaja baadhi ya maeneo yanahusu sekta za fedha na sheria ya bima katika kipindi cha mageuzi ya kiuchumi.

Prof. Kanywanyi, aliyejiunga na utumishi wa UDSM kwa mara ya kwanza mwaka 1967, katika utumishi wake aliwahi kuwa Mkuu wa Kitivo cha Sheria ambacho sasa kinaitwa Shule Kuu ya Sheria UDSM, kwa vipindi vitatu tofauti jumla yake miaka 12.

Kwa mujibu wa Prof. Khoti Kamanga, moja wa watendaji waandamizi wa shule hiyo sheria, historia hiyo inamweka marehemu Prof. Kanywanyi kuwa na rekodi kipekee, mbali na zingine zinazomwingiza katika safu ya wanasheria nguli barani Afrika.

Mwaka 2017, wakati anatimiza miaka 50 ya utumishi UDSM, marehemu Kanywanyi aliandika kitabu kinachoelezea wasifu na historia yake alichokiita ‘My Journey from Family to University in Faith Searching for God’.

Habari Kubwa