Profesa Nyagori ashauri Taasisi za Afya kumpatia tuzo Rais Magufuli

25Jun 2020
Christina Haule
Morogoro
Nipashe
Profesa Nyagori ashauri Taasisi za Afya kumpatia tuzo Rais Magufuli

​​​​​​​DAKTARI Mshauri Mwandamizi wa Magonjwa ya Ndani na Moyo kutoka katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Profesa Harun Nyagori, ametoa ushauri kwa Taasisi za Vyuo Vikuu vya Afya nchini, pamoja na Shirika la Afya Duniani (WHO), kumpatia tuzo maalumu ya heshima, Rais Magufuli,-

-kwa ajili ya kutambua mchango wake katika mapambano dhidi ya janga la Corona.

Profesa Nyagori ambaye pia ni Mhadhiri wa vyuo vikuu mbalimbali vya tiba, amesema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Morogoro, huku akisema kuwa ipo haja ya kutambua mchango mkubwa uliotukuka alioutoa Rais Magufuli kufuatia mbinu za kipekee alizozitumia kupambana na janga la mlipuko wa ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na Virus vya corona.

“Nikiwa kama mtaalamu niliyebobea katika masuala ya tiba ya maradhi ya binadamu kwanza ninampongeza sana Rais Dkt. Magufuli, kwa namna alivyoweza kutoa mchango wake mkubwa kwa watanzania na Ulimwengu kwa ujumla katika kupambana na janga la mlipuko wa ugonjwa wa Corona na ninatoa wito kwa taasisi za vyuo vikuu vya Afya hapa nchini na Shirika la Afya la Duniani (WHO) kumpatia tuzo maalumu Rais Magufuli kwa kutambua mchango wake.” Amesema Profesa Nyagori.

Aidha, Profesa Nyagori ambaye amewahi kutunukiwa tuzo mbalimbali za kimataifa zilizotambua mchango wake katika tafiti za maradhi ya moyo Barani Afrika, amesema kuwa ugonjwa wa Corona ulipoingia  kwa mara ya kwanza hapa nchini, wananchi wengi walijawa na hofu kubwa juu ya athari za ugonjwa huo na hivyo walihitaji sana kumpata mtu wa kuwatoa hofu hiyo.

“Msongo wa mawazo (stress) unasababisha uwezo wa kinga mwilini kushindwa kupigana na maradhi na hivyo kinga za mwili kupungua ambapo kichocheo cha corticosteroid kinachozalishwa kwenye mwili kinaweza kuwa kisababishi kikubwa cha kupunguza kinga za mwili… hofu huchukua nafasi kubwa sana katika kumfanya mtu kupata athari kubwa za ugonjwa Fulani” Amesema Profesa Nyagori.

Profesa Nyagori pia amezungumzia kuhusu mbinu ya kujifungia ndani (karantini) kama njia ya kuepuka na kuepusha kusambaa kwa maambukizi ya virusi vya Covid-19, amesema endapo kama ingetumika, ingelikuwa na madhara makubwa kuliko faida.

“Hatua ya Rais Magufuli kutokubaliana na mbinu ya kujifungia ndani (Lockdown), imesaidia sana katika kuwafanya watanzania kuendelea kutafuta fedha ambazo zimewawesha kumudu kupata milo yenye lishe ambayo kimsingi imeimarisha kinga zao na kufanya isiwe rahisi kushambuliwa na maradhi ya Corona”

“Kujifungia ndani licha ya kisaikolojia kuongeza wasiwasi, lakini pia humfanya mtu kutopata fursa ya kutafuta pesa na hivyo kutomudu kupata mahitaji muhimu ikiwemo vyakula mchanganyiko ambavyo ni muhimu kwa lishe inayoimarisha kinga ya mwili.” amesema Profesa Nyagori.

Habari Kubwa