Programu ya IIdea yawanufaisha wanawake, vijana 25,000

18Nov 2019
Daniel Sabuni
Arusha
Nipashe
Programu ya IIdea yawanufaisha wanawake, vijana 25,000

WANAWAKE na vijana 25,000 kutoka katika Nchi sita za Jumuiya ya Africa Mashariki (EAC) wamefaidika na miradi mbalimbali ya ujasiriamali kutoka Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Ujerumani (Giz) kupitia programu ya IIdea.

Kaimu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Africa Mashariki Christophe Bazivumo akiongea na waandishi wa Habari mara baada ya kuzindua kikao cha siku nne, cha wadau wa Nchi wanachama wa EAC.Picha na Daniel Sabuni, Arusha

Joiyce Kimaro, Mshauri Mkuu wa Programu ya IIdea, amesema wananchi hao wamewezeshwa kwa kubuni wazo la biashara ambalo linahusisha au kugusa sekta mbili zilizomo ndani ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Amesema mawazo hayo yalipitishwa kwenye programu hiyo iliyoanza kutekelezwa Mwaka 2016  na kupatiwa elimu ya biashara husuani masoko na jinsi kufanya biashara na kupata faida, kukuza mtaji na kupunguza changamoto za kimaisha zinazokabili familia na jamii zao.

"Tunapoona wazo la biashara limekidhi vigezo tunawapa sasa elimu na hata mtaji kulingana na biashara anayoifanya, tunatoa hadi  Dola za Kimarekani 5,00 kwa kikundi,"amesema Kimaro

Amesema Pia programu ya IIdea inatekeleza miradi kwenye sekta za afya, Kilimo, biashara na utalii.

Kimaro ametaja Nchi kunakotekelezwa Miradi ya Programu hiyo kuwa ni Tanzania, Burundi, Rwanda, Kenya, Uganda na Sudani Kusini.

Baadhi ya wadau waliofaidika na Programu hiyo kutoka Tanzania wamesema mwanzo walikuwa fukara na mtaji mdogo kuongeza kuwa miradi iliyowezeshwa imewainua kiuchumi katika familia na jamii kwa ujumla.

Mary Ngulupa, mfanyabiashara wa urembo, kutoka mji mdogo wa Namanga mpakani mwa Tanzania na Kenya amesema programu ya IIdea imewasaidia kuwapatia elimu na kukuza mtaji kwa wanawake na vijana katika biashara za shanga, mazao ya kilimo kama ya mahindi na maharage.

"Mimi mwanzoni nilikuwa ha mtaji mdogo baada ya kuwezeshwa nimekuza mtaji na kuweza kutosheleza familia yangu kwa mahitaji ya lazima ya chakula na malazi"amesema Ngulupa.

Amesema nimeweza kusomesha watoto wanne shule za mchepuo wa Kingereza na mmoja amemudu kumlipia kijana wake ada ya chuo kiasi cha pesa ya kesho 30, 000 na sasa yuko mwaka wa tatu wa mwisho kumaliza masomo Nchini Kenya katika fani ya uhasibu.

Naye Mary Wuantent kutoka Namanga upande wa Kenya, amesema akianza na mtaji wa shilingi 3000 za Kenya, sasa anapata faida ya shilingi 1000 ya Kenya kwa siku na anamudu kulipa karo ya shilingi 4000 kwa temu kwa watoto wawili wanosoma shule ya Kira Kira Nchini humo.

Aidha ameitaka IIdea kuwatafutia masoko ya Nchi ya Afrika Mashariki ili kuweza kupanua soko, kupata pesa za kigeni na faida zaidi ili wakuze mitaji iwe na uwezo na sura ya Kimataifa na kukidhi hadhi ya Kimataifa.

IIdea imekuwa kwenye utekelezaji wa Programu yake katika miradi 25 iliyoanza miaka 3 iliyopita tangu 2016 na Ilizinduliwa na Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo Balozi Liberat Mufumukeko wakati wa Kikao cha 5 cha Jumuiya ya EAC  jijini Bunjubura 2017.Miradi iliyoanzishwa imeweza kufaidisha watu 25, 000.

Habari Kubwa