Programu yaja kuwezesha kutambua corona kwa simu

26May 2020
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe
Programu yaja kuwezesha kutambua corona kwa simu

TAASISI ya Utoaji Huduma za Afya Aga Khan (AKHS) kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Aga Khan (AKU), wamezindua programu mpya kwenye simu itakayosaidia watu kutambua kirahisi dalili za corona wakiwa nyumbani na hatua za kufuata.

Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Aga Khan, Sisawo Konteh, katika taarifa yake jana, alisema programu hiyo ijulikanayo kama ‘CoronaCheck’ itaweza kupakuliwa bure kupitia simu za android na iPhone.

“Programu hii imetengenezwa na kituo cha rasilimali za afya dijiti cha mtandao wa maendeleo wa Aga Khan katika jitihada za kuunga mkono juhudi za serikali kupunguza kuenea kwa ugonjwa wa corona,” alisema.

Konteh alisema sehemu kubwa ya changamoto ya corona inabadilika kwa namna wanavyofikiria kuhusu ugonjwa huo.

“Kwa kutumia programu (App), unaweza kutambua kwa haraka dalili za ugonjwa na kutafuta msaada wa kitabibu na kupima kuondoa hofu, wasiwasi, imani potofu na unyanyapaa kupitia jukwaa la ubunifu la dijiti,” alisema.

Alisema programu hiyo inatumia mazungumzo ya maingiliano, ikiendeshwa na teknolojia inayoruhusu mtumiaji kuelewa dalili zake na kutambua kama tayari ameshapata maambukizo ya corona na kutafuta msaada kwa wakati.

Pia, Konteh alisema inalenga kutambua vitu vinavyoweza kubeba virusi vya corona na kupunguza uwezekano wake kusambazwa.
“Programu hii pia inaorodhesha namba za kitaifa za usaidizi wa haraka, nambari za usaidizi zinapatikana kwa kumbukumbu rahisi.

“Kifaa hiki kimepitishwa kutoka kwa huduma za afya za Alberta na kikaboreshwa kukidhi mahitaji ya nchini kwetu kwa kuangalia mlipuko wa ugonjwa.”

Alisema utaalamu wa kiteknolojia wa kukuza programu umetolewa na Kituo cha Teknolojia na ubunifu cha AKU (TISC).

Mkurugenzi, Kituo cha Teknolojia na Ubunifu cha AKU, Saleem Sayani, alisema CoronaCheck inatoa fursa ya kupunguza mzigo katika mfumo wa afya.

“Matokeo yetu ya awali yanaonyesha kuwa asilimia 19 ya watumiaji walihitaji upimaji wa haraka na msaada wa matibabu.

“Hii ilisaidia kupungua kwa idadi ya watu waliokuwa wakitembelea vituo vya afya hivyo kuhakikisha rasilimali muhimu kama vifaa vya upimaji pamoja na wakati wa wahudumu wa afya kutumika kwa wale waliokuwa na uhitaji wa lazima.”

Alisema CoronaCheck inalenga pia kuondoa imani potofu na upotoshaji kwa kuhusisha video za kielimu ili kukabiliana na ongezeko la idadi ya taarifa ambazo hazijathibitishwa zinazozunguka kwenye mitandao ya kijamii.

Pia, inahusisha taarifa zilizothibitishwa kuhusu njia bora za kujikinga na maambukizo na ushauri wa namna ya kujitathmini.

Kadhalika, alisema inahusisha tahadhari na mwongozo wa kuepuka mikusanyiko uliopendekezwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) pamoja na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

Habari Kubwa