PSSSF yataja sababu nne  mafao ya wastaafu kuchelewa

03Aug 2021
Abdallah Khamis
Mtwara
Nipashe
PSSSF yataja sababu nne  mafao ya wastaafu kuchelewa

MENEJA Matekelezo wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa watumishi wa umma nchini, (PSSF),Victor Kikoti, ameeleza sababu nne zinazochangia mafao ya wafanyakazi wa mfuko huo kuchelewa kulipwa na kuwafanya wastaafu waishi katika mazingira magumu wakati wakisubiria mafao yao.

Meneja Matekelezo wa mfuko wa hufadhi ya jamii kwa watumishi wa Umma,Victor Kikoti,akifafanua jambo kwa waandishi wa habari Mkoani Mtwara,baada ya ufunguzi wa semina ya siku mbili kwa watumishi wanaitarajia kustaafu katika mwaka wa fedha wa 21/22. (Picha na Abdallah Khamis)

Kikoti ametoa kauli hiyo leo mkoani Mtwara, alipomuwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa PSSF Hosea Kishimba, kwenye semina ya siku mbili kwa watumishi wa umma wanaotarajia kustaafu katika mwaka wa fedha wa 21/22.

Amezitaja sababu hizo kuwa ni waajiri kuchelewa kufunguliwa kwa wakati madai ya wafanyakazi wao wanaoratajia kustaafu, Wafanyakazi kutokujaza taarifa zao kwa usahihi, michango yote ya  wanaotarajiwa kustaafu kutokuwasilishwa kwenye mfuko mpaka muda wa kustaafu unapofika na wastaafu kuingia katika mikopo umiza.

Kuhusu kuchelewa kufungua madai, Kikoti amesema  kwa mujibu wa sheria ya mfuko wa hifadhi ya jamii kwa watumishi wa umma kipengele cha 43, mwajiri anatakiwa kuuandikia mfuko huo  juu ya matarajio ya kustaafu kwa mfanyakazi wake na kisha kumsaidia kujaza  fomu kwa usahihi kabla ya kuzifikisha kwenye mfuko ndani ya miezi sita kabla ya kustaafu.

“Sisi hatupokei fomu kutoka kwa mfanyakazi, bali fomu inaletwa na mwajiri,lakini hapa pia kunakuwa na mapungufu mengi ya ujazaji,kwa kuwa baadhi ya waajiri wanakuwa hawajakamilisha michango  yote ya mfanyakazi husika lakini mfanyakazi hajui hilo”amesema Kikoti.

Ameongeza kuwa asilimia kubwa ya wastaafu fomu zao zinajazwa baada ya kustaafu hali inayofanya wachelewe kupata mafao.

Ameeleza kuwa sheria inawataka kukamilisha malipo ya mfanyakazi aliyestaafu ndani ya siku 60, tokea kustaafu, hivyo ni wajibu wa waajiri kuhakikisha wafanyakazi wao hawapati usumbufu baada ya kumaliza utumishi wa umma kwa mujibu wa sheria.

Kuhusu mikopo umiza kuchelewesha malipo ya wastaafu, Kikoti alisema wengi wa wafanyakazi wanaokaribia kustaafu, na wale  waliochelewa kujaziwa fomu kwa mujibu wa sheria na taratibu za mfuko, huingia katika mikopo yenye riba kubwa na taasisi zisizo rasmi, hali inayochangia  kufanyika kwa uhakiki zaidi kabla ya malipo yao kufanyika.

“Tumeona hili la mikopo isiyo rasmi ndiyo maana tumealika taasisi za fedha waje kutoa elimu hapa, lakini ushauri wangu ni vema wastaafu wanapopata mafao yao wakawekeza kwenye vitu vitakavyowazalishia kwa uhakika ikiwemo ununuzi wa hati fungani kwenye mabenki” amesema Kikoti.

Ameongeza licha ya changamoto hizo kwa sasa PSSF,imefungua ofisi 29 katika mikoa yote  nchini na kuandaa mifumo ya malipo kwa mfumo wa kidigitali, utakaowasaidia wanachama kuona taarifa zao mapema hali itakayowafanya warekebisha pale penye kasoro kwa ajili ya kuharakisha malipo muda wa kustaafu utakapofika.

Awali mkuu wa mkoa wa Mtwara, Brigedia Jenerali,Marco Gaguti, akifungua mafunzo hayo ya siku mbili, aliwataka watumishi wanaokaribia kustaafu,wahakikishe wanakuwa na mipango mizuri ya kimaisha ili wasiwe wategemezi kwa watu wengine baada ya kustaafu.

Brigedia Jenerali Gaguti, amesema kustaafu katika kazi ya kuajiriwa isiwe mwisho wa utumishi wa wananchi kwa maslahi ya Taifa na kwamba ni vema watu hao wakajiepusha na kila jambo litakalokuwa na mlengo wa kuwaangusha kimaisha.

Popote tutakapokuwa tunapaswa tutumie uzoefu wetu wa kazini kuisaidia jamii,tuhakikishe hatuwi changamoto kwa wengine, maana mafao ya mara moja huwa ni mtihani kwa walio wengi kuwa na matumizi sahihi  na endelevu” amesema Brigedia Jenerali Gaguti

Habari Kubwa