Puma yapiga "jeki" upasuaji watoto wenye matatizo ya moyo

30Sep 2019
Mary Geofrey
Dar es Salaam
Nipashe
Puma yapiga "jeki" upasuaji watoto wenye matatizo ya moyo

WATOTO 20 wenye matatizo ya moyo ambao wanahitaji kufanyiwa upasuaji katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), wamepatiwa msaada wa matibabu.

Msaada wa Sh. milioni 40, imetolewa leo na Kampuni ya Mafuta ya Puma kwa ajili ya kuwezesha upasuaji kwa watoto hao kati ya 500, wanaohitaji msaada huo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo, Dominic Dhanah, amesema wametoa fedha hizo kuunga mkono jitihada za Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, katika kuwasaidia watoto hao.

Amesema kampuni yake siku zote ipo tayari kushirikiana na Serikali katika masuala ya kijamii ndiyo sababu imeona ipo haja ya wao kushiriki kuwasaidia watoto hao. “Sisi tunafanya biashara lakini jamii inayotuzunguka tunaipa kipaumbele na ndiyo maana siku zote tuko tayari kushiriki na kusaidia shughuli mbalimbali na hawa watoto tumeona tuna wajibu wa kushiriki kuokoa maisha yao,” amesema Dhanah.

Kwa upande wake Makonda mbali na kuishukuru Puma kwa msaada huo, amesema mwanzoni  mwa Oktoba ataunda  kamati ya kutafuta Sh. bilioni moja ambazo zitafanikisha upasuaji wa watoto wote 500.

“Nataka kufikia Disemba  watoto hawa  wawe wamefanyiwa upasuaji na kupata matumaini ya kuuona mwaka mpya wakiwa na matumaini ya kuishi,” amesema Makonda.

Sambamba na hilo, Makonda ameipongeza kampuni hiyo kwa kuratibu mafunzo ya usalama barabarani kwa wanafunzi wa shule za msingi na kueleza kuwa imesaidia kupunguza vifo vinavyotokana na ajali kwa kundi hilo.

“Kwa miaka sita ambayo Puma imetoa mafunzo haya kwa watoto tunaona vifo vinapungua, mwaka huu amefariki mtoto mmoja tu na wengine wanne kujeruhiwa. Takwimu hizi zinaonyesha ni kiasi gani watoto wanaelewa matumizi sahihi ya barabara na niwaombe watu wazima hasa waendesha bodaboda muendelee kuwasaidia ili wawe salama,” amesema Makonda.

Katika shindano la mwaka huu, mwanafunzi wa darasa la tano katika Shule ya Msingi Kibamba, Emmanuel aliibuka mshindi wa mchoro bora na alipata kitita cha Sh. 500,000.

Sambamba na zawadi hiyo Emmanuel ameiwezesha shule yake kupata vocha ya Sh. milioni 4, kwa manunuzi ya vifaa vya maktaba.

Habari Kubwa