Puma yatoa mafunzo ya usalama barabarani kwa wanafunzi 80,000

18Mar 2019
Mary Geofrey
DAR ES SALAAM
Nipashe
Puma yatoa mafunzo ya usalama barabarani kwa wanafunzi 80,000

JUMLA ya wanafunzi 80,000 wamepatiwa mafunzo ya usalama barabarani katika kipindi cha miaka mitano.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhandisi Hamad Masauni akimpa zawadi mmoja wa Wanafunzi wa shule ya msingi Bunge jijini Dar,mara baada kujibu vizuri swali lililohusu mambo ya usalama barabarani,kabla ya ufunguzi rasmi wa mafunzo ya Usalama barabarani yanayotolewa na Kampuni ya Puma Energy Tanzania iishirikiana na wadau wengine ikiwemo taasisi ya AMEND.

Mafunzo hayo yametolewa na Kampuni ya mafuta ya Puma katika shule 75 nchini kwa lengo la kupunguza ajali za barabarani hasa kwa wanafunzi wa shule za msingi.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni, ameyasema hayo wakati akizundua awamu ya sita ya mafunzo hayo katika kuelekea kongamano la wiki ya usalama barabarani litakalofanyika Machi 30, mwaka huu.

Amesema mafunzo hayo na uchoraji wa picha za usalama barabarani kwa wanafunzi  wa shule za msingi yana lengo la kuwapa uelewa wa kukabiliana na tatizo la ajali barabarani.

“Elimu ni suala la kipaumbele kwa jamii na mkakati wetu ni kupunguza ajali za usalama barabarani na Puma inafanyakazi hii kwa karibu na Machi 30, mwaka huu tutakuwa na kongamano la wiki ya usalama barabarani pia tujadili hili kwa kina,” amesema Masauni.

Mwanafunzi Shule ya Msingi Bunge jijini Dar, Omari akifafanua kuhusu namna ya matumizi sahihi kwa watembea kwa miguu mbele ya Mgeni rasmi Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani nchi ( wa tatu kulia ) Mhandisi Hamad Masauni,wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya Usalama barabarani yanayotolewa na kampuni ya Puma Energy Tanzania.

Amesema Serikali inafarijika na kazi inayofanywa na Kampuni ya Puma kwa kurudisha faida inayopatikana kwa jamii ikiwamo kutoa mafunzo muhimu ya usalama barabarani hasa kwa wanafunzi ambao ni taifa la kesho.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Puma, Dominic Dhanah, amesema kuwa mafunzo hayo yanakwenda sambamba pia kwa wanafunzi waliowahi kufundishwa.

Amesema madhumuni ya kuwahusisha wanafunzi wa shule za msingi, wanaamini kuwa watoto hao wanakabiliwa na hatari za ajali za barabarani na kuhitaji mafunzo ya usalama barabarani ili kuepuka ajali.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi Mhandisi Hamad Masauni akiwaaaga baadhi ya wanafunzi ambao ni pia ni Mabalozi wa Usalama barabarani wa shule ya msingi Bunge jijini Dar,mara baada ya kufungua rasmi mafunzo ya Usalama barabarani yanayotolewa na kampuni ya Puma Energy Tanzania kishirikiana na wadau wengine ikiwemo taasisi ya AMEND.

“Usalama barabarani ni kipaumbele namba moja katika Kampuni ya Mafuta Puma na tumeamua kuwafundisha watoto wadogo kwani tunfahamu hatari za barabarani wanazokabiliana nazo.

“Tumefanya utafiti na kugundua kuwa shule tulizoendesha mafunzo haya , ajali kwa wanafunzi zimepungua na hivyo basi kwa mwaka 2019 mafunzo haya yataendeshwa katika mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma na Zanzibar,” amesema Dhanah

Habari Kubwa