Punda chanzo ajali ya Mwigulu

14Feb 2019
Ibrahim Joseph
Dodoma
Nipashe
Punda chanzo ajali ya Mwigulu

MBUNGE wa Iramba Magharibi (CCM), Dk. Mwigulu Nchemba, jana alipata ajali iliyosababishwa na punda watatu waliokuwa wakikatiza barabara huku wakikimbizana.

Baadhi na Madaktari na Wauguzi katika Hospitali ya Benjamin Mkapa, wakishauriana jambo baada ya kumpokea Mbunge Irimba Magharibi, Mwigulu Nchemba aliyepata ajali ya gari katika eneo la Migoli mkoani Iringa na kukimbiwa hospitalini hapo, jijini Dodoma jana. PICHA: IBRAHIM JOSEPH

Dk. Nchemba alisema hayo akiwa katika Hospitali ya Benjamin Mkapa alikolazwa baada ya kupata ajali hiyo katika kijiji cha Mtera, huku Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Kamishna Msaidizi (ACP) Juma Bwire, akithibitisha hivyo.

Akizungumza na waandishi wa habari, Nchemba alisema ajali hiyo ilitokea majira ya saa 2.45 asubuhi katika eneo hilo akitokea Iringa kwenda mkoani Singida kwenye kikao wa Kamati ya Siasa ya Mkoa.

Alisema wakiwa njiani katika eneo hilo, punda watatu walikatisha katika barabara hiyo ambayo dereva wake alijitahidi kuwakwepa lakini ilishindikana na kumgonga mmoja wao.

“Tulikuwa tunatoka Iringa kwenda Singida kwenye kikao cha Kamati ya Siasa (ya CCM) Mkoa, tulipofika eneo la Migori, ghafla nikaona punda wanakatisha barabara. Dereva alijaribu kuwakwepa na kufanikiwa kuwakwepa wawili lakini huyo mmoja ilishindikina ikabidi amgonge, hicho ndicho chanzo cha ajali,” alisema Nchemba.

“Nilisikia mlio mkali ndani ya gari sikuelewa ni nini lakini nikawa natafuta namna ya kufungua mkanda ili nitoke nje. Baada  ya hapo niliona moshi mwingi ndani ya gari nikamuuliza dereva mbona kuna moshi naye alimjibu kuwa hajui. Nilifanikiwa kufungua mkanda wa gari na kutafuta namna ya kutelemka,” alisema.

Dk. Nchemba alisema baada ya kujua kuwa hali zao ziko vizuri alimshauri dereva watelemke isije ikawa gari linataka kuwaka moto kutokana na ajali iliyotokea.

“Tulifanikiwa wote kutoka kwenye gari tukiwa salama huku nikijisikia maumivu kifuani,tumboni na kwenye kiuno lakini nilikuwa najitambua, nikaanza kuwajulisha ndugu zangu kuwa nimepata ajali,” alisema.

Kwa mujibu wa Dk. Nchemba alibebwa na gari la serikali lililokuwa likienda Dodoma hadi Hospitali ya Benjamin Mkapa kwa ajili ya matibabu.

“Kwa kweli nimepokewa vizuri timu ya madaktari na wauguzi na kuanza kupatiwa matibabu haraka,” alisema na kuwatoa hofu wananchi kuwa anaendelea vyema na madaktari wamesema hakuna tatizo kubwa.

DEREVA ASIMULIA

Akizungumzia mazingira ya ajali hiyo, dereva wake, Johnson Malesi alisema ajali ilitokana na punda alipokuwa akiwakwepa ili asiwagonge.

“Tulikuwa tumekimaliza kijiji na tulikuwa eneo la wazi ambalo si makazi ya watu. Ghafla lilitokea kundi la punda waliokuwa wakivuka barabara kwa kasi, hivyo kusababisha ajali,” alisema.

"Nilisikia kishindo nilimgonga punda mmoja kati yao nilipogeuka pembeni nilimuona mheshimiwa amelala akaniuliza vipi, nikamjibu nipo salama. Basi tukafungua mikanda kushuka chini akawa analalamika anasikia maumivu," aliongeza.

Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Muungano na Mazingira, Mussa Sima, alisema alipata taarifa hiyo akiwa njiani kutoka Morogoro na kuamua kufika hospitalini hapo ili kumjulia hali.

“Nimezungumza naye nashukuru Mungu anajitambua na kwa taarifa ya madaktari inaonekana hajapata madhara makubwa,”alisema.

DAKTARI ALONGA

Kwa upande wake, Mkurungenzi wa Hospitali ya Benjamin Mkapa Dk. Alphonce Chandika alisema walimpokea Mbunge huyo majira ya saa 3:30 asubuhi baada ya kupata ajali.

Dk. Chandika alisema baada ya kupokewa, mgonjwa alichukuliwa vipimo vya CT-Scan, X-ray na Utra Sound lakini alikuwa akilalamika maumivu kifuani, tumboni na kwenye kiuno.

Hata hivyo, alisema baada ya vipimo kutoka vilionyesha kuwa hakupata mivunjiko sehemu yoyote  ya mwili wake na ilionekana michubuko sehemu za tumboni na kwamba inawezekana ni mkanda wa gari ulisababisha.

“Tumeamua kumlaza kwanza mgonjwa ili kuendelea kuchukua vipimo kila baada ya muda na akiendelea vizuri ataruhusiwa kurudi nyumbani. Hali yake ni nzuri msiwe na wasiwasi,” alisema Chandika.

TAARIFA YA POLISI

Akizungumzia ajali hiyo, Kamanda Bwire alisema Dk. Nchemba alipata ajali hiyo saa 2:00 asubuhi katika kijiji cha Mtera katika eneo la changarawe mkoani Iringa baada ya gari yake kugonga punda waliokuwa wakikimbizana barabarani.

“Ni kweli Mbunge wa Iramba, Mwigulu Nchemba amepata ajali majira ya saa mbili asubuhi katika kijiji cha Mtera katika eneo la changarawe. Dereva wake aligonga punda ambao walikuwa wakikatiza barabarani wakikimbizana,” alisema Kamanda Bwire.

Alisema Dk. Nchemba aliumia katika mguu wa kulia na kwamba alikuwa akienda mkoani Dodoma kwa shughuli za kikazi.

“Dereva wake aliyekuwa akiendesha gari la mbunge huyo namba T 246 DNN Land Cruiser V8 anaitwa John Richard, hakuumia isipokuwa mbunge ndiye aliyeumia kwenye mguu wa kulia na pia gari limeharibika sana,” alisema Kamanda Bwire na kuongeza:

“Lakini tunashukuru kwamba wote wako salama na taratibu za kumkimbiza kwenda Dodoma kwa ajili ya matibabu zilifanyika  kwa haraka.”

Habari Kubwa