Pwani, TADB sasa kuwainua wakulima

27Nov 2020
Julieth Mkireri
Kibaha
Nipashe
Pwani, TADB sasa kuwainua wakulima

MKOA wa Pwani kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), imeweka mpango wa  kuwainua wakulima kiuchumi, ambapo wakulima 3,000 wananufaika kwa pembejeo. 

Wakulima hao wanaolima mpunga katika bonde la Mto Ruvu Halmashauri ya Chalinze wilayani Bagamoyo Mkoa wa Pwani,  watanufaika na pembejeo za kilimo.

Hayo yalibainishwa na Mkuu wa Mkoa huo, Mhandisi Evariost Ndikilo, wakati wa makabidhiano ya  mkopo  wa matrekta mawili pamoja na  pembejeo nyingine za kilimo  zenye thamani ya  shilingi milioni 480 kwa uongozi wa Chama cha Ushirika  wa Wakulima wa Umwagiliaji wa Ruvu (CHAURU) ambavyoo vimetolewa na TADB.

Pia aliahidi kuwa katika kufanikisha azma ya mradi wa bonde la Mto Ruvu, ataendelea kuwapa ushirikiano wa kutosha wakulima wa mazao mbalimbali ukiwamo mpunga na kuwahimiza wadau wengine wa sekta ya kilimo kuunga juhudi za serikali katika kuwasaidia wakulima kutimiza malengo waliyojiwekea.

Mkurugenzi wa Fedha wa TADB, Delick Lugemala, ambaye  alimwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, alisema lengo lao ni kuwakomboa wakulima kwa kuwapatia mikopo kwa bei nafuu, na kwamba katika Mkoa wa Pwani wameshatoa zaidi ya shilingi bilioni 20.

Alisema benki hiyo itaendelea kushirikiana na wakulima kwa kuwezesha mitaji, ambayo watakuwa wanaipata kwa riba nafuu, lengo ni kuwapatia fursa mbalimbali za kilimo, ambazo zitawasaidia katika kujipatia kipato na kujikwamua kiuchumi.

Mwenyekiti wa Bodi ya CHAURU, Sadala Chacha, alisema msaada huo utawaondolea vikwazo vya upatikanaji wa zana za kilimo na kuwaondolea usumbufu waliokuwa wanaupata awali.

Habari Kubwa