Qatar Airways kuendelea kutoa huduma bora

22Jan 2022
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Qatar Airways kuendelea kutoa huduma bora

SHIRIKA la Ndege la Qatar Airways limetangaza kuongeza wigo wa safari za ndege katika nchi mbalimbali duniani, sambamba na kuendelea kutoa huduma bora kwa wasafiri wake.

Wafanyakazi wa shirika la ndege la Qatar Airways wakishika bango kuonyesha miaka 15 tangu waanza kusafirisha watu kutoka Doha mpaka Dar es Salaam.

Taarifa iliyotolewa na shirika hilo, ilieleza kuwa pia linajivunia kutimiza miaka 15 ya kutoa huduma Tanzania tangu liliopoanza rasmi Januari 9, 2007 kwa safari kutoka Dar es Salaam hadi Mji Mkuu wa Qatar, Doha.

Makamu wa Rais wa Qatar Airways Afrika, Hendrik Dupreez, alisema katika taarifa hiyo kuwa wanajivunia kwa miaka hiyo kuitumikia Tanzania na kuunganisha nchi na mtandao wao wa kimataifa.

Alisema maadhimisho ya miaka 15 yanaimarisha zaidi uhusiano wa Qatar na Tanzania na uwezo mkubwa ambao njia ya Dar es Salaam imekuwa na mafanikio sana.

“Tunatarajia miaka mingi zaidi kuwaunganisha wasafiri kutoka sehemu mbalimbali duniani, ili kujionea utamaduni na wanyamapori wa kipekee Tanzania,” alisema Dupreez.

Alisema Qatar Airways itaendelea kushirikiana na wafanyabiashara na wasafiri wa burudani kuendelea kuwafikisha sehemu mbalimbali wanazokwenda katika bara la Afrika, Ulaya, Asia na Amerika.

Mbali  na usafirishaji abiria, alisema Qatar Airways inasafirisha bidhaa na mizigo kama vile dawa, vifaa vya teknolojia, samaki, nyama na maua kwenda mahali kwenye mtandao, hususani katika nchi za Hong Kong, Uholanzi.

Dupreez alisema Qatar Airways kwa sasa inaendelea kujenga upya mtandao wake na kwamba kwa sasa ina zaidi ya vituo 140 duniani vikiwamo Zanzibar na Kilimanjaro.

Katika sehemu ya kusherehekea miaka 15, Qatar Airways ilifanya tafrija katika Uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) kwa wafanyakazi wake kugawa zawadi mbalimbali kwa abiria waliokuwa katika ndege QR 1499 na QR 1476.

Habari Kubwa