Rada mpya kufungwa mikoa mitatu

24Mar 2020
Renatha Msungu
Dodoma
Nipashe
Rada mpya kufungwa mikoa mitatu

WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe, amesema katika kuboresha huduma za hali ya hewa nchini, serikali imenunua rada tatu ambazo zitafungwa katika mikoa ya Mtwara, Mbeya na Kigoma.

WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe, picha mtandao

Akizungumza jana jijini hapa kwenye kilele cha maadhimisho ya Siku ya Hali Hewa Duniani yaliyofanyika katika Ofisi za Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Kamwelwe, alisema baada ya kufungwa rada hizo kutakuwa na mtandao wenye rada tano, ambazo zitakuwa na uwezo wa kuliona anga la Tanzania kwa asilimia 70.

Alisema kutokana na uwekezaji wa serikali katika sekta ya hali ya hewa nchini, huduma zinazotolewa na mamlaka hiyo kwa sasa zimeendelea kuongeza viwango vya ubora pamoja na usahihi wa utabiri.

Waziri huyo alisema kwa sasa usahihi wa utabiri wa hali ya hewa upo kati ya asilimia 88 na 96, viwango ambavyo ni juu ya viwango vinavyokubalika ambapo viwango vya kimataifa ni asilimia 70.

“Haya ni mafanikio makubwa katika kutekeleza sera na mikakati ya serikali ya awamu ya tano sambamba na kutekeleza mkataba wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), hivyo natoa wito kwa wadau wote wa hali ya hewa kushiriki shughuli za maendeleo za sekta hii,” alisema Kamwelwe.

Aidha, Waziri Kamwelwe alisema, uboreshaji wa huduma hiyo utasaidia kukabiliana na majanga mbalimbali, yakiwamo mafuriko na vimbunga.

“Taarifa za hali mbaya ya hewa zinapotolewa kwa wakati huwezesha serikali kukabiliana na majanga hayo,” alisema.

Alisisitiza kuwa serikali itaendelea kuboresha mtandao wa vituo vya ufuatiliaji na upimaji wa hali ya hewa nchini, utabiri wa hali ya hewa kwa ajili ya matumizi ya maamuzi katika sekta mbalimbali ikiwamo ya maji, kilimo na uchukuzi ili kuhakikisha serikali na wananchi wanapata taarifa sahihi.

Kadhalika, Kamwelwe alisema miongoni mwa mambo muhimu ambayo serikali imetekeleza katika kuboresha huduma ya sekta hiyo ni pamoja na kutunga Sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Namba 2 ya Mwaka 2019.

“Sheria hii inaiwezesha TMA kutekeleza majukumu yake kitaifa, kikanda na kimataifa katika kutoa huduma kwa ubora na ufanisi zaidi. Aidha, sheria hii inaipa TMA nguvu ya kudhibiti huduma za hali ya hewa zinazotumiwa kibiashara,” alisema.

Habari Kubwa