RAHCO yataka waliojenga eneo la reli kupisha 

03Dec 2017
Ibrahim Joseph
Nipashe Jumapili
RAHCO yataka waliojenga eneo la reli kupisha 

Baadhi ya Wafanyabiashara waliokuwa wakifanya biashara katika maeneo ya stendi ya daladala ya mabasi yaendayo Mikoani katika  manispaa ya Dodoma  wameanza kuvunja majengo na vibanda vyao chini ya ulinzi wa askari polisi ili kupisha ujenzi wa reli ya kisasa.

Hatua hiyo imetokana na Kampuni hodhi ya rasilimali za reli (RAHCO) kuwataka watu wote waliopo kwenye hifadhi ya reli kupisha eneo hilo.

Nipashe ilishuhudia wafanyabiashara hao wakihamisha mali zao na kuvunja vibanda vyao huku kukiwa na ulinzi mkali.

Mmoja wa wafanyabiasha hao Alia Antony alisema pamoja na kuvunja huko lakini hawakupewa taarifa za kuhama katika eneo hilo hadi walipotakiwa kuhama.

Antony alisema wao hawapingi kuondoka ila kitendo cha kuhamishwa huku wakiwa na biashara zao na wengine wana mikopo kwenye taasisi za kifedha watashindwa kulipa kutokana kukosa maeneo ya kufanyia biashara.

Maeneo mengine yaliyokumbwa na bomoa bomoa hiyo ni pamoja na kituo cha kukatisha tiketi cha mabasi ya shabiby na vituo vikubwa vya mafuta vya Orxy na Total vyote vipo kwenye eneo la reli.