Raia Cameroon ahukumiwa faini mil. 100/-

05Mar 2020
Hellen Mwango
Dar es Salaam
Nipashe
Raia Cameroon ahukumiwa faini mil. 100/-

RAIA wa Cameroon Johnson Table (32), amehukumiwa kulipa faini ya Sh. milioni 100 au kwenda jela miaka mitatu baada ya kupatikana na hatia ya kukutwa na Dola za Marekani 84,300 bila maelezo.

Raia wa Cameroon, Johnson Table, akiwa chini ya ulinzi wa askari Polisi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam jana, kabla ya kuhukumiwa kulipa faini ya Sh. milioni 100 au kwenda jela miaka mitatu, baada ya kupatikana na hatia ya kukutwa na Dola za Marekani 84,300 bila maelezo. PICHA: MIRAJI MSALA

Kadhalika mahakama hiyo imetaifishwa Dola za Marekani 84,300 alizokutwa nazo kuwa mali ya serikali baada ya mshtakiwa kukiri kosa la kukutwa na fedha hizo bila maelezo.

Hukumu hiyo ilisomwa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam iliyoketi chini ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Rashidi Chaungu.

Table alilipa faini hiyo na kuachiwa huru.

Awali, Wakili wa Serikali Mwandamizi Wankyo Simon, akisaidiana na Wakili wa Serikali Mkuu, Shadrack Kimaro, alimsomea mshtakiwa mashtaka yake na kukiri.

Kimaro aliomba mahakama pamoja na adhabu ya kulipa faini, fedha za kigeni alizokutwa nazo zitaifishwe kuwa mali ya serikali.

Wankyo, alidai kuwa Februari 27, mwaka huu, katika Uwanja Ndege wa Julius Nyerere, uwanja namba tatu, mshtakiwa akiwa safarini kutoka nchini alikutwa na Dola za Marekani 84,300 bila maelezo kwa Mamlaka ya Forodha ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania.

Baada ya kusomewa mshtakiwa alikiri makosa na kusomewa maelezo ya awali dhidi ya mashtaka yanayomkabili.

Mshtakiwa ambaye ni mfanyabiashara na mkazi wa Linde, Cameroon, aliingia nchini Februari 26, mwaka huu, kwa mujibu wa kumbukumbu zilizopo Mamlaka ya Forodha, wakati anaingia nchini hakueleza kama anaingia na fedha zozote.

Februari 27, alikuwa akiondoka nchini kupitia ndege ya Rwanda na alikuwa na tiketi ya kielekitroniki pamoja na hati ya kusafiria.
Ndege hiyo ilikuwa ikiondoka saa 11.40 jioni kuelekea Kigali na baadaye Duoala, Cameroon.

Mshtakiwa alikuwa ameshika begi, akiwa uwanjani alianza utaratibu wa kuingia na akapita kwenye mashine ya kwanza ya ukaguzi, alipoenda kwenye mashine ya pili ili aingie kwenye chumba cha kusubiria abiria, kitu kisicho cha kawaida kiligundulika katika begi lake.

Inadaiwa alielekezwa aache mkoba wake kwenye mashine kwa mara ya pili na kitu kisicho cha kawaida kilibainika.

Ilidaiwa kuwa aliamriwa kutoa kila kitu kilichokuwa kwenye begi, fedha hazikuwa miongoni mwa vitu vilivyotolewa.

Begi lilipowekwa kwenye mashine ilibaika kuwa ndani zilifichwa fedha na lilipopekuliwa ilibainika Dola za Marekani 84,300.
Fedha zilizokamatwa ziliwekwa kwenye akaunti katika Benki ya NMB na namba zake zilinakiliwa.

Inadaiwa kumbukumbu za Uhamiaji zinaonyesha kuwa mshtakiwa aliingia nchini Februari 26, 2020 kama mtalii na kupewa viza ya utalii, hakutembelea kituo chochote cha utalii na alipoingia nchini hakueleza kama alikuwa na fedha za Marekani.

Ushahidi ulikua unaonyesha wazi kuwa mshtakiwa alikuwa anaondoka nchini bila kueleza Mamlaka ya Forodha fedha alizokuwa nazo.

Habari Kubwa