Raia wa Uganda, Rwanda wakamatwa pori la akiba

10Dec 2016
Anceth Nyahore
SHINYANGA
Nipashe
Raia wa Uganda, Rwanda wakamatwa pori la akiba

RAIA wa Rwanda na Uganda wamedaiwa kukamatwa katika hifadhi ya misitu wa Kigosi Myowosi iliyoko katika mikoa ya Shinyanga, Geita na Kigoma wakiwa na mifugo hivyo kusababisha uharibifu mazingira.

Sambamba na kuharibu mazingira katika hifadhi hiyo, hali hiyo imeelezwa kuchangia uharibifu wa vyanzo vya maji katika Mto Malagarasi mkoani Kigoma na Mto Nyikonga, Geita na kusababisha mabadiliko ya tabia nchi katika ukanda wa mikoa ya Kanda ya Ziwa na Magharibi.

Meneja wa mapori hayo, Patrick Kutondolana, alisema idadi kubwa ya mifugo hasa ng’ombe inayokutwa katika mapori ya akiba ya Kigosi Myowosi, inatoka Rwanda na Uganda na baadhi ya Watanzania wachache wanaokamatwa kwenye maeneo hayo kwa kuhusika kula njama za kuwapokea wahamiaji hao haramu.

Alisema wachungaji wengi wanaokamatwa katika mapori wanazungumuza lugha za mataifa ya Rwanda na Uganda, hali ambayo
inaashiria kuwa ni raia wa nchi hizo na haijulikani kama kuna watu wanawaingiza Meneja huyo alisema makundi makubwa ya mifugo hukutwa ndani ya mapori hayo na hali hiyo na kusababisha wanyamapori kuhama baada ya mazingira wanayoishi kutokuwa rafiki kwao.

Alisema na kutahadharisha kuwa endapo hali hiyo haitadhibitiwa inaweza kusababisha wanyamapori kutoweka na kusababisha watalii kuacha kuingia katika mapori hayo.

Pia alisema hata wamiliki halali wa vitalu vya uwindaji na upigaji picha wanaweza kukata tamaa kuwekeza na hata kuhama kutokana na kukosa wanyama wa kuwinda na kupigaji picha.

Kutondolana alisema licha ya uharibifu wa mazingira pia kumekuwapo na tatizo sugu la ujangili unaosababisha uwindaji wa
wanyamapori vivutio ndani ya hifadhi hizo kama vile tembo, digidigi na nyati ambao huwindwa sana hali ambayo
huenda ikachangia watalii kutoingia katika hifadhi hiyo.

Katika kukabiliana na hali hiyo, meneja huyo alisema wanatarajia kufanya vikao na wakuu wa kambi za wakimbizi
ili kuwaelimisha jinsi ya kukabiliana na tatizo hilo kwa kuwa wanaokamatwa wengi wao ni wakimbizi.

Habari Kubwa