Rais ashangaa kupuuzwa, kutoheshimiwa sheria

18Mar 2019
Rahma Suleiman
ZANZIBAR
Nipashe
Rais ashangaa kupuuzwa, kutoheshimiwa sheria

RAIS wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, ameonya kuwa licha ya kuwapo kwa sheria tisa zinazohusiana na matumizi bora na endelevu ya ardhi, bado watu hawaziheshimu wala kuzifuata.

RAIS wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein.

Akizungumza wakati akifungua semina kuhusu masuala ya ardhi na mali zisizorejesheka iliyofanyika mjini Unguja, alisema lengo la kuhakikisha ardhi inatumika vyema limeifanya serikali kutunga sheria tisa kuhusiana na matumizi bora na endelevu ya rasilimali hiyo.

Alizitaja baadhi ya sheria hizo kuwa ni ya Matumizi ya Ardhi Na. 12 ya Mwaka 1992, Sheria ya Uhaulishaji wa Ardhi Na. 8 ya Mwaka 1994 na Sheria ya Mahakama ya Ardhi Na. 7 ya Mwaka 1994, ambayo ndiyo inayohusiana na uanzishwaji wa mahakama hiyo.

Dk. Shein alisema katika ziara yake aliyoifanya katika wilaya zote za Unguja na Pemba mwezi uliopita amefahamu mengi kuhusiana na kadhia ya kuvunjwa kwa sheria mbalimbali zinazohusiana na matumizi bora ya ardhi.

Alieleza kuwa kwa bahati mbaya wavunjaji wa sheria hizo ni viongozi na watendaji wa serikali na matukio mengine yanayofanywa na wananchi wa kawaida.

“Taarifa za wilaya zilizowasilishwa kwangu zote zimethibitisha kuendelea kuibuka kwa migogoro mipya ya ardhi katika wilaya iko ya uvamizi wa maeneo ya serikali, mingine ni baina ya wananchi na wawekezaji,” alisema Dk. Shein.

Aidha, alieleza kuwa jambo jingine ni kuwapo kwa uharibifu mkubwa wa mazingira katika maeneo yanayochimbwa mchanga aliyoyatembelea ikiwa ni pamoja na kuwapo kwa upungufu wa mchanga wenyewe.

Alieleza kuwa katika maeneo aliyoyatembelea katika ziara yake hiyo yakiwamo Donge Chechele, Pangatupu na Kiombamvua kwa Unguja na Finya (Selem) na Shumba Viamboni kwa upande wa Pemba, amejionea hali halisi ya mchanga na kusisitiza kuwa ni mali ya serikali hivyo ni rasilimali ya wote.

Unguja mchanga umepungua kwa kiasi kikubwa tena haupo isipokuwa kuna maeneo sita bado upo, lakini ni maeneo ya kilimo ambayo wananchi wanalima mazao mbali mbali ya chakula, hivyo kunatakiwa maamuzi ya kuendelea na kilimo au kuchimbwe mchanga ambao utachimbwa kwa wastani wa mwaka na nusu, alisema.

Alieleza kuwa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira Na.3 ya Mwaka 2015, pamoja na kanuni zake inafahamisha kwamba mchimbaji mchanga anatakiwa apate kibali, achimbe kwa kuzingatia kima maalum na aingie mkataba wa kurejesha eneo katika hali ya kawaida kama kupanda miti baada ya kumaliziza uchimbaji.

Dk. Shein alieleza kuwa utekelezaji wa sheria hiyo umekosa usimamizi na matokeo yake maeneo mengi yaliokwisha kuchimbwa mchanga yamebaki kuwa majangwa na miti iliyopandwa haikustawi kama ilivyokusudiwa.

Alieleza kuwa takwimu zinaonyesha kwamba yapo magari 750 Unguja na 165 Pemba yanayobeba mchanga na kwamba ni nyingi mno kwa shughuli hiyo na kati ya gari hizo zipo zenye uwezo wa kuchukua hadi tani 30, ambazo nazo kwa kipindi kirefu zimekuwa zikichangia uharibifu wa miundombinu ya barabara.

Dk. Shein alisisitiza haja ya kufanywa kwa utafiti kama anavyosisitiza mara kwa mara katika uongozi wake kwa lengo la kukabiliana na changamoto zilizopo katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo.

Alieleza kuwa kwa kutumia tafiti ndipo itawezekana kuwapo kwa mipango imara ya matumizi ya rasilimali zilizopo sambamba na kuwa na mipango na njia mbadala za kutumia pale inapolazimika kufanya hivyo.

Waziri wa Ardhi, Nyumba, Maji na Nishati, Salama Aboud Talib, alisema kuwa semina hiyo itasaidia kujua hali halisi iliyopo kuhusu ardhi na mali zisizorejesheka Zanzibar.

Habari Kubwa