Rais afichua madudu mifuko ya jamii

29Dec 2018
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Rais afichua madudu mifuko ya jamii

RAIS John Magufuli, ameanika madudu ndani ya mifuko ya jamii ambayo yalisababisha mzigo mkubwa kwa serikali hata kufikia hatua ya kushindwa kuwalipa wanachama wao baada ya kustaafu.

RAIS John Magufuli, picha na mtandao

Magufuli alisema hayo jana Ikulu, Dar es Salaam, katika mkutano wake na viongozi wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta), vyama shiriki, viongozi wa mifuko ya hifadhi ya jamii (PSSSF na NSSF), Mamlaka ya Usimamizi wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE).

Alisema mifuko hiyo ilikuwa na mizigo mikubwa ya madeni ambayo ilisababisha wastaafu kushindwa kulipwa kwa wakati hali ambayo ilisababisha serikali kuingilia kati.

Rais alibainisha kuwa mifuko hiyo ilikuwa na deni la makato ya wafanyakazi yaliyofikia Sh. trilioni 1.23 ambalo lilisababisha wastaafu kukwama kulipwa mafao yao.

Kutokana na deni hilo, Rais alisema serikali ililibeba deni hilo na hadi sasa imeshalipa Sh. bilioni 550 kati ya Sh. Bilioni 774 walizokuwa wakidai huku waliobaki wakiendelea kulipwa kadiri uhakiki unavyofanyika.

Mbali na madeni hayo, Rais Magufuli alisema mifuko hiyo iliwekeza katika miradi isiyo na tija ambayo ilikuwa mzigo kwa wanachama na kuwanufaisha wachache wakiwamo watendaji, wakurugenzi wa bodi na baadhi ya wanasiasa.

Alitolea mfano wa mradi wa nyumba wa Dege Eco Village, Kigamboni jijini Dar es Salaam ambao ulifanywa na lililokuwa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) ambao alisema haufai na umeingiza hasara kubwa.

“Mradi kama ule ni mfano wa uwekezaji usio na tija. Haufai hata kidogo na ulipaswa kufanywa na watu binafsi wanaojua masuala ya real estate (milki) na si mfuko wa jamii,” alisema.

Alisema miradi ya uwekezaji kama hiyo haizalishi na kuleta matokeo chanya kwa wadau badala yake watu wachache ndio wanaonufaika nayo.

Rais alitaja madudu mengine kuwa ni matumizi aliyoyaita ya ovyo yaliyokuwa yakifanywa ndani ya mifuko hiyo.

“Mfuko mmoja wa hifadhi ya jamii (hakuutaja jina) ulikuwa ukichapisha kalenda, vitu vya ‘promotion’ (vipeperuhi) na ‘sponsorship’ (udhamini) kwa Sh. bilioni 1.3. Huu ni mfano wa matumizi ya ovyo,” alisema na kuongeza:

“Tena mfuko huo umeajiri walinzi ‘very expensive’ (kwa gharama kubwa) kwa Sh. bilioni mbili kwa mwaka. Kama wangeajiri Suma JKT gharama zake zingekuwa hata chini ya Sh. bilioni moja kwa mwaka.”

Alisema gharama kama hizo zingepunguzwa, fedha zingekuwapo zikiwamo za kuwalipa wastaafu na kwamba hata hiyo kanuni ya mafao isingekuwa tatizo.

Pia alisema mifuko hiyo imekuwa ikitumia gharama kubwa hata katika uendeshaji jambo ambalo limesababisha fedha nyingi kutumika vibaya wakati wanachama ambao ndio wanufaika wakiwa wanakosa hata pemsheni zao.

Habari Kubwa