Rais azuia wananchi kuondolewa mpaka wa hifadhi ya Serengeti

17Oct 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Rais azuia wananchi kuondolewa mpaka wa hifadhi ya Serengeti

RAIS Samia Suluhu Hassan amezuia wananchi kuondolewa katika eneo kinga (buffer zone) la Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ili kutafuta suluhu ya mgogoro wa muda mrefu kati ya hifadhi na wakazi wa vijiji 14 vinavyozunguka hifadhi hiyo.

Hifadhi ya Taifa ya Serengeti iliyoko mkoani Mara, ilisogeza mipaka ya eneo lake la kinga kwa zaidi ya mita mia tano katika maeneo ya vijiji katika mbuga kwa wilaya za Serengeti na Tarime na kuwafanya wakazi wake kuishi kwa hofu na kushindwa kujua hatima yao.

Vijiji vilivyonufaika na uamuzi wa Rais Samia kwa upande wa wilaya ya Serengeti ni Bisarara, Bonchugu, Nyamakendo, Nyamburi, Machochwe, Mbalibali na Merenga na wilaya ya Tarime ni Gibaso, Kegonga, Kenyamosabi, Nyandage, Nyabirongo, Karakatonga na Masanga.

Uamuzi huo ulitangazwa juzi na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, kwa niaba ya Kamati ya Mawaziri Wanane wa wizara za kisekta katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Bisarara.

Kamati hiyo ya mawaziri iko katika ziara ya kutembelea mikoa mbalimbali kwa ajili ya kutoa mrejesho wa uamuzi wa Baraza la Mawaziri kuhusu utatuzi wa migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji 975.

Hata hivyo, wananchi wa vijiji hivyo wametahadharishwa kuwa na subira mpaka timu ya wataalamu itakapokwenda kubainisha mipaka na kuwekwa kwa mpango wa matumizi bora ya ardhi katika maeneo hayo.

Waziri Lukuvi ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Mawaziri wa Wizara za Kisekta, alisema serikali kupitia Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, ilichukua eneo la vijiji 14 katika wilaya hizo kwa ajili ya eneo kinga ya hifadhi na Rais ameridhia mamlaka hiyo irudishe nyuma mipaka yake ili ardhi itumiwe na wananchi.

"Mama (Rais) anawapenda sana na anajua kuna migogoro midogo midogo ya ardhi lakini kwa sasa ametaka mpokee uamuzi huu kama salamu na hataki shida na wananchi wake wateseke kwa jambo moja kwa muda mrefu," alisema Lukuvi.

Waziri Lukuvi aliwaambia wakazi wa vijiji hivyo kuwa wamepakana na hifadhi namba moja duniani, hivyo zawadi pekee watakayompatia Rais kwa uamuzi huo ni wao kuimarisha ulinzi katika eneo la hifadhi ili mbuga iwe salama.

Wananchi wa kijiji cha Bisarara waliupokea uamuzi wa kupatiwa ardhi katika eneo la Hifadhi ya Serengeti kama ukombozi baada ya kuishi kwa hofu na manyanyaso kwa muda mrefu.

Zakaria Petro, mkazi wa Bisarara, alisema uamuzi huo utawafanya wananchi wa vijiji hivyo kuishi kwa amani. Alisema awali walikuwa wanasumbuliwa na mamlaka ya hifadhi kwa kukamatwa na wakati mwingine mifugo yao kuchukuliwa.

Naye Mniko Constantino mkazi wa Mugumu, Serengeti, aliahidi kumlipia gharama ya kuchukulia fomu ya kugombea urais Samia katika uchaguzi wa mwaka 2025 kutokana na hatua mbalimbali anazochukua kwa kipindi kifupi cha uongozi wake ikiwamo kuwapatia ardhi wananchi wanaoishi katika vijiji vilivyokuwa maeneo ya hifadhi.

Mbunge wa Jimbo la Serengeti, Dk. Amsabi Mrimi, alimshukuru Rais Samia kwa uamuzi wa kuwajali wananchi wa vijiii hivyo na kueleza kuwa mtu anayetoa ardhi kwa wananchi anakuwa amewasaidia kwa kuwa ardhi ndiyo kila kitu.

Aliiomba serikali kufanya mrejesho wa sheria ya kuhamisha mifugo katika maeneo ya vijiji vilivyoko kando ya hifadhi kwa kuwa sheria hiyo imesababisha madhara makubwa kwa jamii ya wafugaji.

Habari Kubwa