RAIS MAGUFULI ALA KIAPO, AAHIDI KUKUZA UCHUMI

05Nov 2020
DODOMA
Nipashe
RAIS MAGUFULI ALA KIAPO, AAHIDI KUKUZA UCHUMI
  • Katika hutuba yake mara baada ya kuapishwa, Rais Dk. Magufuli ameahidi kukuza uchumi akizingatia ajira kwa vijana na kujenga mahusiano ya kimataifa

Rais John Pombe Magufuli na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan wamekula kiapo asubuhi ya leo tarehe 5 Novemba 2020 mbele ya Jaji Ibrahim Hamisi Juma katika mji mkuu wa Dodoma.

Katika hotuba yake baada ya kuapishwa, Rais Magufuli ameahidi kuendeleza uhusiano wa kimataifa na kukuza uchumi akizingatia kuongeza ajira kwa vijana

Sherehe hiyo inamfanya kuwa rais wa kwanza wa Tanzania kuapishwa katika mji mkuu wa Dodoma.

Waliohudhuria ni pamoja na Rais wa Zanzibar Hussein Ali Mwinyi, Mama Anna Nyerere, mke wa Baba wa Taifa hayati Mwalimu Julius Nyerere pamoja na marais wa zamani Ali Hassan Mwinyi na Jakaya Kikwete pamoja na wajumbe wa marais kutoka kote ulimwenguni.

Pia waliohudhuria hafla hio ni pamoja na marais wa nchi jirani Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda, Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe na Azali Assoumani wa Comoros.

Walikuwepo pia wanadiplomasia kutoka Ethiopia, Kuwait, Qatar, EU, China na Marekani kati ya wengine wengi.

Katika hotuba yake, Rais wa Uganda Yoweri Museveni alimpongeza rais Magufuli na kuwapongeza watanzania wote kwa kumaliza uchaguzi kwa amani.

Rais Museveni alitoa pia hongera kwa mafanikio ya Tanzania kufika uchumi wa kati na kusema nchi yake nayo ipo mbioni kufikia hatua hiyo.

Katika hutuba zao, Rais Museveni, Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe na Rais Azali Assoumani wa Comoro wote wamehimiza umoja wa Afrika na kumpa heshima kubwa hayati Baba wa taifa Mwalimu Julius Nyerere kwa kazi aliyoifanya kujenga umoja wa Afrika.

 

Tanzania ilipiga kura tarehe 28 Oktoba na Tume ya Uchaguzi ya Taifa (NEC) ikamtangaza Rais John Pombe Magufuli kuwa mshindi baada ya kupata kura milioni 12.5 ambayo ni sawa na asilimia 84.

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Muungano wa Tanzania inaundwa na Tanzania Bara na Visiwani Zanzibar ambapo Dk Hussein Ali Mwinyi alichukua urais baada ya kupata asilimia 76 ya kura.

Je! Unajua ni vipi vipaumbele vya maendeleo vya Rais Magufuli? Endelea kutufuatilia: https://epaper.ippmedia.com

 

Habari Kubwa