Rais Magufuli kufungua maonyesho ya SITE

18Oct 2019
Dotto Lameck
Dar es Salaam
Nipashe
Rais Magufuli kufungua maonyesho ya SITE

Rais Dkt John Magufuli anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye ufunguzi wa maonesho ya Swahili International Tourism Expo (SITE) kesho Oktoba 19, 2019 katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.

Rais Dkt John Magufuli.

Akizungumza na waandishi wa habari, Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Prof Adolf Mkenda amesema maonyesho hayo yameanza leo Oktoba 18 na kumalizika Oktoba 20 mwaka huu ambapo kesho Oktoba 19 yatafunguliwa rasmi na Rais Magufi.

Amesema kuwa lengo la maonyesho hayo ni kuwaunganisha wafanyabiashara wadogo na wakati wa utalii nchini pamoja na wafanyabiashara kutoka masoko makuu ya utalii duniani.

"SITE imeendelea kupata mafanikio makubwa kila mwaka ambapo ni jambo la kujivunia kama Wizara, wadau wa sekta ya utalii  na nchi kwa ujumla kuona onyesho hili linaendelea kukua mwaka hadi mwaka na kuvutia washiriki wengi kutoka kila kona ya dunia" amesema Mkenda.

Aidha, ameeleza kuwa TTB imeandaa ziara kwa ajili ya Mawakala wa Utalii na Waandishi wa habari wa Kimataifa Oktoba 21, kwenda kutembelea maeneo mbalimbali ya vivutio vya asili ikiwemo Hifadhi ya Taifa Serengeti na Mamlaka ya Hifadhi ya Bonde la Ngorongoro.

Pia ametaja maeneo mengine ni Fukwe za Tanga na Mapango ya Amboni, Misitu ya Magoroto, Mlima Kilimanjaro na miradi ya utalii wa utamaduni katika Mkoa wa Kilimanjaro, Hifadhi ya Taifa ya Riaha na Mji wa Iringa

Pia Hifadhi ya Taifa ya Udzungwa na Mikumi, Visiwa vya Zanzibar na Mafia.

Habari Kubwa