Rais Ndayishimiye aipongeza CRDB

25Oct 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Rais Ndayishimiye aipongeza CRDB

BENKI ya CRDB imepongezwa kwa kufanikisha kuimarika kwa ushirikiano wa kibiashara kati ya Tanzania na Burundi kupitia huduma zake za kibenki.

Akizungumza jijini Dodoma mwishoni mwa wiki baada ya kuweka jiwe la msingi la uijenzi wa kiwanda cha Itracom Fertilizers Limited cha wawekezaji kutoka Burundi, Rais Evariste Ndayishimiye alisema, Benki ya CRDB imekuwa mshirika mkubwa wa kuimarisha biashara na uwekezaji baina ya nchi hizo mbili. Benki ya CRDB imetoa mkopo wa kuwezesha ujenzi wa kiwanda hicho cha mbolea.

“Uwezeshaji uliofanywa na benki katika ujenzi wa kiwanda hiki cha mbolea ni ushahidi tosha wa namna gani benki imejikita katika kufanikisha kuimarika kwa biashara na uwekezaji baina ya nchi zetu zenye udugu wa karibu,” Rais Ndayishimiye alisema.

Alisema uwekezaji huo wa raia kutoka nchini kwake, utawezesha kiwanda cha mbolea cha Itracom kuzalisha tani 600,000 kwa mwaka na kutoa ajira kwa Watanzania wasiopungua 10,000.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mkuu na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela, alisema benki yake yenye matawi matatu nchini Burundi imekuwa ikitoa mikopo kwa miradi mbalimbali ya kimkakati ya serikali ya Burundi na Tanzania. Benki inatarajia kufungua tawi la nne wilayani Gitega mwaka huu.

Nsekela alisema benki yake inafanya biashara kwa muda mrefu na wawekezaji wa Itracom huko Burundi kwa kuwapatia huduma zote za kibenki. Miongoni mwa miradi ambayo benki imefadhili Burundi ni pamoja na ujenzi wa kiwanda cha mbolea cha Fomi na kiwanda cha saruji huko Rutana ambacho benki imetoa mkopo wa Dola za Marekani milioni 10.

“Mheshimiwa Rais, uwapo wako hapa leo kuweka jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda cha Itracom ni ushahidi tosha wa kuimarika kwa uhusiano baina ya Burundi na Tanzania. Kama benki ya kizalendo yenye mtazamo wa kimataifa, Benki ya CRDB ina mkakati wa makusudi wa kuwezesha kuimarika kwa uhusiano ya kibiashara na uwekezaji baina ya nchi za Afrika ya Mashariki ili kukuza uchumi na kuboresha maisha ya watu,” alisema.

Kadhalika, alisema benki hiyo imeshawekeza mtaji wa Dola milioni 107 nchini Burundi katika sekta mbalimbali za uchumi wa nchi hiyo ukiwamo mradi wa kuzalisha umeme wa maji Mpanda.

Benki hiyo pia imewezesha kampuni ya Itracom kuwekeza katika kiwanda cha mbolea cha Minjingu kilichoko Babati mkoani Manyara. “Hapa nchini Tanzania benki yetu imewezesha kampuni ya Itracom kwa kuipatia mkopo wa dola 12 milion kwaajili ya ujenzi wa kiwanda cha Minjingu kilichopo Babati,” Nsekela alisema.

Tangu ianzishe kampuni tanzu nchini Burundi mwaka 2011, Benki ya CRDB imetoa mchango mkubwa katika ujenzi wa taifa kupitia kutoa ajira kwa Warundi na pia kulipa kodi mbalimbali za serikali kufanikisha maendeleo.

Habari Kubwa