Rais Nigeria afungwa miaka 30 kwa kukutwa na dawa za kulevya

22Jun 2019
Hellen Mwango
Dar es Salaam
Nipashe
Rais Nigeria afungwa miaka 30 kwa kukutwa na dawa za kulevya

MAHAKAMA Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, imemhukumu kifungo cha miaka 30 jela raia wa Nigeria, Christian Ugbechi, baada ya kukutwa na hatia ya kusafirisha pipi 56 za dawa za kulevya aina ya Heroin Hydrochloride.

Christian Ugbechi.

Aidha, mahakama hiyo imeagiza pipi alizokutwa nazo mtuhumiwa ziharibiwe kwa mujibu wa sheria.

Hukumu hiyo ilisomwa jana katika mahakama hiyo chini ya Jaji Sirrilius Matupa  baada ya kusikiliza ushahidi wa watu 11 na vielelezo 22 kutoka upande wa Jamhuri dhidi ya mshtakiwa.

"Bila kuacha shaka, mahakama yangu baada ya kupitia ushahidi na vielelezo vya upande wa Jamhuri, imeridhika na ushahidi wa Jamhuri kweli alitenda kosa hilo na inamtia mshtakiwa hatiani," alisema Jaji Matupa.

Pia alisema kwa mujibu ya kifungu cha 15 kidogo cha (1) cha Sheria ya Udhibiti Dawa za Kulevya, mshtakiwa atakwenda jela kutumikia kifungo cha miaka 30 na pipi alizokutwa nazo ziliteketezwe kwa mujibu wa sheria.

Mapema Juni 19, mwaka huu, mshtakiwa alikutwa na hatia kabla ya kutolewa adhabu hiyo jana.

Hata hivyo, Jaji alisema pamoja na mshtakiwa kujitetea kwamba alifanyiwa upekuzi mara tatu na hakukutwa na kitu chochote, hivyo upande wa Jamhuri  ulipaswa kuleta ushahidi wa CCTV, haikuwa lazima kuwapangia  mashahidi wa kuwaleta na kwamba walikuwapo mashahidi wengine waliothibitisha mashtaka dhidi yake.

Alisema Mkemia Mkuu wa Serikali katika uchunguzi wake, amethibitisha dawa za kulevya alizozichunguza ndizo alizokutwa nazo mshtakiwa huyo.

Kabla ya kusomwa kwa adhabu Jaji Matupa alitoa nafasi kwa Jamhuri kutoa hoja.

Wakili wa Serikali, Constantine Kakula, alidai kuwa hawana kumbukumbu ya makosa ya nyuma ya mshtakiwa, lakini aliiomba mahakama itoe adhabu kali iwe fundisho kwa watu wakiwamo raia wa nje wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya.

Wakili wa  utetezi, Jeremiah Ntobesya, aliomba mahakama kumpunguzia adhabu mteja wake kwa sababu ana mke na watoto wawili wanaomtegemea na pia mshtakiwa anasumbuliwa na matatizo ya moyo na kwamba amekaa gerezani kwa mwaka mmoja na nusu na kipindi hicho chote alikuwa na tabia njema.

Pia alisema, pamoja na kwamba kifungu cha sheria kinaamuru mshtakiwa kuhukumiwa kifungo cha maisha gerezani, lakini siyo lazima, itolewe adhabu hiyo, mahakama inaweza kuamua vinginevyo.

Mapema mahakamani hapo, katika ushahidi wake, askari wa upelelezi kutoka Kituo cha  Uwanja wa Ndege, Konstebo Peter alidai kuwa aliandika maelezo ya mshtakiwa huyo na katika mahojiano alimweleza kuwa amemeza pipi za dawa za kulevya.

Alidai baada ya kueleza hayo alimweka mahabusu ili kuzitoa na kwamba hadi  Januari 30, 2018 saa 10:30  jioni alitoa pipi 23 alizomeza.

Pia alidai walichukua kielelezo hicho na pipi zingine zilizokutwa kwenye begi na kuzipeleka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali ambapo kwa pamoja zilikutwa na uzito wa gramu 947.17.

"Matokeo ya uchunguzi yalionyesha kuwa pipi zote zilikuwa ni dawa za kulevya ambazo ni Heroin Hydrochloride zilizochanganywa na Paracetamol Metronidazole na Papavirine," alidai Peter.

Mkuu wa Kituo cha Uwanja wa Ndege, Inspekta Dickson Haule, alidai siku ya tukio majira ya saa 8:00 mchana akiwa ofisini alijulishwa na askari huyo wa upelelezi kuwa kuna mtuhumiwa amekamatwa na dawa za kulevya.

Haule alidai baada ya taarifa hiyo alienda Ofisi ya Polisi Interpol walipokuwa na alishuhudia mtuhumiwa akipekuliwa  ndipo aliona begi dogo la mgongoni kuna pipi 56 zikiwa zimeviringishwa ndani ya soksi mbili nyeusi.

Katika kesi hiyo, inadaiwa Januari 28, mwaka jana maeneo ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Ilala mkoani Dar es Salaam, mshtakiwa alikutwa akisafirisha dawa hizo zenye uzito wa gramu 947.57.

Habari Kubwa