Rais Samia akonga nyoyo za walimu

19Dec 2021
Na Mwandishi Wetu
Nipashe Jumapili
Rais Samia akonga nyoyo za walimu

RAIS Samia Suluhu Hassan amesema anazifahamu kero za walimu hivyo atazifanyia kazi na amewapongeza kwa kazi nzuri wanayofanya.

Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako (kushoto) akizungumza na Rais Samia Suluhu Hassan (picha ya kusanifu) kwenye mkutano mkuu wa wakuu wa shule za sekondari nchini uliofanyika Mlimani City. Rais aliwaambia walimu kwa njia ya simu kwamba anajua changamoto zao na atazitatua.

Alitoa ahadi hiyo mwishoni mwa wiki wakati alipozungumza nao kwa njia ya simu kwenye ufungaji wa mkutano wa wakuu wa shule za sekondari.

Mkutano huo wa siku tatu uliratibiwa na Global Education Link (GEL) na Umoja wa Walimu wa Shule za Sekondari ( TAHOSSA), ulifanyika Mlimani City.

Rais Samia alimpigia simu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye ufungaji wa mkutano huo. 

Rais Samia alisema alipanga kuhudhuria mkutano huo lakini hakufanikiwa kutokana na majukumu makubwa aliyonayo. 

Mratibu wa mkutano huo wa wakuu wa shule za sekondari  Abdulmalik Mollel ambaye ni Mkurugenzi wa Global Education Link (GEL) akizungumza wakati wa kufunga mkutano huo maeneo ya Mliman City jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.

"Ilikuwa niwe nanyinyi lakini sikuweza kutokana na kutingwa na majukumu natambua issues zenu nitazifanyia kazi,  " alisema Rais Samia na kusababisha  walimu kulipuka kwa furaha 

Mbali na hayo, Rais Samia alisema anatambua kazi kubwa na nzuri inayofanywa na walimu na aliwapongeza huku akiwataka waendelee kuchapa kazi.

Rais Samia aliwahakikishia walimu hao wakiwemo viongozi wa chama chao TAHOSSA ambao aliwataja kwa majina kuwa serikali itaendelea kumaliza changamoto zinazowakabili.

Baadhi ya viongozi wa TAHOSSA wakiwa wamesimama kumsalimia mgeni rasmi Waziri Profesa Ndalichako alipofunga mkutano wao mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Profesa Ndalichako aliwataka walimu wazingatie miongozo wanapotoa adhabu kwa wanafunzi.

Alisema baadhi ya walimu wamekuwa wakitoa adhabu kinyume na miongozo na taratibu kiasi cha kuwafanya wanafunzi kuzichukia shule.

Alisema baadhi ya shule zimekuwa zikiwakatalia wanafunzi kwenda likizo kwa kisingizio cha masomo ya ziada na kuwalazimisha kulipia masomo hayo.

Waziri Ndalichako akiserebuka na walimu mara baada ya kufunga mkutano wao wa siku tatu Mliman City jijini Dar es Salaam.

Alisema  amekuwa akipata malalamiko mengi kutoka kwa wazazi kwa wanafunzi kuzuiwa kwenda nyumbani wakati wa likizo. 

Alisema likizo ni haki ya msingi ya mwanafunzi kwani anahitaji mapumziko ya kutembelea ndugu jamaa na marafiki na kama kuna ulazima wa masomo ya ziada wapate kibali kutoka kwa maofisa elimu.

" Tusigeuze shule kuwa Magereza, yaani mwanafunzi akianza kidato cha kwanza harudi nyumbani hadi kidato cha nne hapana. Sote tumesoma na tunakumbuka tulivyokuwa tunarudi nyumbani lkizo," alisema 

Sehemu ya wakuu wa shule za sekondari nchini wakimsikiliza Profesa Ndalichako wakati akifunga mkutano wao Mliman city jijini Dar es Salaam.

Habari Kubwa