Rais Samia, Museveni kuinua uchumi, ajira

28Nov 2021
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Rais Samia, Museveni kuinua uchumi, ajira

​​​​​​​RAIS wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan na Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, wamekubaliana mambo saba yenye lengo la kuinua uchumi na kutoa ajira kwa wananchi wa nchi hizo mbili.

Rais Samia Suluhu Hassan, akisalimiana na mgeni wake, Rais wa Uganda, Yoweri Kaguta Museveni, baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam jana, kwa ajili ya ziara ya Kitaifa ya siku tatu hapa nchini. PICHA: IKULU

Miongoni mwa mambo hayo ni matumizi ya Bandari ya Dar es Salaam kupitisha shehena la vifaa vya ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Hoima, Uganga hadi Tanga, Tanzania.

Makubaliano hayo yametokana na mazungumzo waliyofanya jana Ikulu jijini Dar es Salaam baada ya Rais Museveni kutua nchini kwa ziara ya siku tatu.

Akizungumza mara baada ya mazungumzo yao, Rais Samia alisema jambo la kwanza walilokubaliana ni kukuza na kuimarisha uhusiano na ushirikiano kati ya nchi hizo mbili.

Alisema wamewaelekeza mawaziri wa sekta kukutana mara kwa mara ili kutatua matatizo yanayojitokeza katika maeneo yao na kuhakikisha ushirikiano huo unaendelea kuimarika.

Rais Samia alitaja jambo la pili kuwa ni ushirikiano katika sekta ya uwekezaji kwa kuwa Uganda ni nchi ya pili katika uwekezaji Tanzania katika ukanda wa Afrika Mashariki, ikiwekeza miradi 45 yenye thamani ya dola za Marekani milioni 114 iliyotoa ajira kwa Watanzania 2,150.

Pia alisema zipo kampuni mbalimbali za Tanzania zilizowekeza nchini Uganda.

Jambo la tatu ni ushirikiano wa biashara, Rais Samia akifafanua kuwa kwa kipindi cha miaka saba biashara kati ya nchi hizo imeendelea kukua, ujazo wa biashara umeongezeka kutoka Sh. bilioni 200 mwaka 2014 hadi Sh. bilioni  607 mwaka 2020.

“Kama mnakumbuka tulikuwa na vikwazo kama hivi Kenya na tulipokwenda na kuwataka mawaziri na wataalamu wakae. Sasa biashara kati ya Tanzania na Kenya imekuwa mara sita zaidi, ni mategemeo yetu tukitatua vikwazo na Uganda, biashara itakua zaidi,” alisema.

Pia alisema wamezungumzia kuhusu ukuaji wa biashara, matumizi ya Bandari ya Dar es Salaam ambapo Rais Museven alieleza hiyo ni aibu mpaka leo bandari hiyo imefikia kusafirisha tani 138,262 kwenda Uganda wakati wanatumia nyingine kwa mamilioni ya tani.

Rais Samia alisema jambo lingine walilolizungumza ni utekelezaji wa kimkakati unaohusisha barabara zinazounganisha nchi hizo na nchi za jirani pamoja na miradi ya umeme wanayoifanya kwa pamoja.

Pia alisema wamezungumzia mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi Afrika Mashariki, mradi wa ICO kutoka Hoima Uganda hadi Tanga ambapo Mei mwaka huu nchi hizo  zilikamilisha utiaji saini  mikataba mbalimbali.

Rais Samia alisema wamekubaliana kushirikiana kuweka kiwanda cha kuzalisha chanjo, zikiwamo za UVIKO-19.

“Chanjo ziwe za UVIKO au chanjo nyingine kwa wanadamu na wanyama, tumewataka wataalamu wetu wakae wajadiliane tutakwenda vipi kwenye kiwanda hiki," alisema.

Pia alisema wamekubaliana mkutano wa kamati ya kudumu ya ushirikiano (JPC) wakutane mwishoni mwa mwezi au mwaka huu kuzungumzia yote yaliyopo kwenye mradi huo.

Rais Museven alisema walikuwa na pendekezo la kukunja vyuma vya bomba la mafuta Tanzania lakini wameona juhudi hizo zinaweza kuchelesha mradi, hivyo wameona kampuni zilizokuwa zimepanga kukunya nje zifanye hivyo.

“Hapa tutakosa ajira Watanzania na Waganda na fedha kiasi lakini acha tuanze, nilipoangalia hesabu ya kujenga bomba hili la mafuta ni dola milioni 1,300.

“Kwa hizo dola milioni 323 ndizo za kununua vyuma vya kutengeneza bomba kuvikunja na kuvipaka rangi. Usafiri kwa bahari ni dola milioni 52. Kizuri wakikunja, kupaka rangi, kusafirisha haziwezi kutumika vizuri bila kuzichoma moto ili vishikane," Rais Museveni alifafanua.

Alisema kiwanda cha kuchoma vyuma hivyo watakijenga Igunga mkoani Tabora na kitagharimu dola milioni 272, usafiri wa ndani dola milioni 43 na kujenga bomba, kuchimba na kuliweka itagharimu dola milioni 684.

Habari Kubwa