Rais Samia abaini mabinti waliobakwa waugua fistula

06Jul 2022
Romana Mallya
DAR ES SALAAM
Nipashe
Rais Samia abaini mabinti waliobakwa waugua fistula

RAIS Samia Suluhu Hassan, ameonyesha kusikitishwa na taarifa kuwa miongoni mwa wagonjwa wanaopokelewa Hospitali ya CCBRT wenye tatizo la fistula ni watoto kuanzia umri wa miaka 11 hadi 12 kutokana na ukatili wa kubakwa.

Rais Samia Suluhu Hassan akiwapongeza na kuwapa zawadi wanawake waliojifungua katika jengo jipya la Huduma ya Afya ya Mama na Mtoto katika Hospitali ya CCBRT, jijini Dar es Salaam jana. PICHA: IKULU

Rais Samia aliambiwa hayo jana jijini Dar es Salaam, wakati akiteta na Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa hospitali hiyo, Brenda Msangi, katika uzinduzi wa jengo la kutolea huduma ya afya ya uzazi, lililojengwa kwa gharama ya Dola za Kimarekani milioni 44 (Sh. bilioni 101.2).

Kiasi hicho kinajumuisha gharama za ujenzi, vifaa na vifaa tiba pamoja na usimamizi ili kumpatia mwanamke huduma bora ya uzazi kuanzia ujauzito, kujifungua na uangalizi wa mama na mtoto.

Akizungumza baada ya uzinduzi huo, Rais Samia alisema, wakati akiteta na Mkurugenzi Mtendaji, alimweleza kuwa umri wa watoto kuanzia miaka 11 hadi 12 ni miongoni mwa wagonjwa wanaowapokea.

“Wana kesi wanazozipokea mtoto wa miaka 12 au 11 analetwa hapa akiwa na fistula na hii inatokana na watoto kubakwa, wale wanaotubakia watoto wanazalisha tatizo hilo, pia kuna vitoto vidogo kabisa miaka minne, mitano, sita wanapokelewa hapa wana tatizo la fistula.

“Ndugu zangu wana jamii tuone tatizo hili la ubakaji ambalo kwa kiasi kikubwa tunalifumbia macho kwenye jamii, hatulisemi hatuwapeleki kunakohusika kwenye vyombo vya sheria wale wanaokosea, matatizo makubwa wanawasababishia watoto wetu wanaowafanyia vibaya.”

Alitaka kupunguzwa idadi ya wagonjwa wanaoishi na fistula Tanzania kwa kuepuka ndoa za utotoni, ubakaji na mimba za mapema.

“Kitoto kina miaka 12 kinapata ujauzito, kitoto miaka 13 kinakuja hapo hakiwezi chochote, amecheleweshwa nyumbani ameanza kusukuma mtoto anachana kila kitu, fistula hiyo tujitahidi kuacha mila ambazo zinaleta matatizo haya,” alisema.

Akizungumzia taarifa alizozipata kutokana na manusura wa vifo vitokanavyo na uzazi baada ya kupata shida wakati wa kujifungua, alisema ndiyo wanaokwenda kama wagonjwa wa fistula na inakadiriwa Tanzania kuwa na wanawake kati ya 12,000 hadi 19,000 wanaoishi na tatizo hilo.

Kuhusu hospitali hiyo, alisema kwa siku inaweza kuhudumia wagonjwa wa nje wanawake 300 na ina jumla ya vitanda 140 na vinane vya kujifungulia.

MUME KUSHUHUDIA MKE KUJIFUNGUA

Rais Samia alisema ndani ya jengo hilo kuna vyumba vinane vinavyomruhusu mzazi kuingia na mwenza wake au ndugu yake wakati wa kujifungua.

“Hakuna wakati wa faraja kama wakati wa kujifungua ukiwa na mtu wako pembeni ambaye anakusaidia kukupooza, hii itasaidia sasa waume zetu kuona kishindo tunachopambana nacho mule ndani, itasaidia waone kinachotokea mule ndani.

“Kwa maana hiyo watasaidia kwenda kwenye uzazi wa mpangilio, watajitahidi kutoa huduma ya kutosha ili siku ikifika mama awe na njia nyepesi ya kumleta mtoto duniani. Mmenifurahisha naamini serikali wataiga mfano huu pia, lazima wale majamaa tuingie nao huko waone kinachoendelea.”

Alisema, hajutii hospitali hiyo kuitwa jina la Samia Suluhu Hassan, kama alivyoombwa.

 

Alisema jengo hilo limeanza kutoa huduma tangu Januari 3, mwaka huu na hadi Juni 10, mwaka huu, jumla ya watoto 65 wamezaliwa, kati ya hao, familia tatu zilipata mapacha na wanawake wawili walikuwa wenye ulemavu ambao walitoka na hali nzuri.

Alisema wakati akitembelea hapo amekuta tatizo la uhaba wa watumishi na alimweleza Waziri Ummy  zinazoweza kuzibika kwa haraka azishughulikie.

AHUZUNISHWA TUKIO BUKOBA

Rais Samia alisema takwimu za vifo vya watoto na wanawake wakati wa kujifungua zinaonyesha asilimia kubwa wanaofariki ni kutokana na upungufu kwa wanaotoa huduma.

“Ama upungufu wa weledi au dharau ya watoa huduma na usimamizi hafifu, hii inanikumbusha kesi iliyotokea juzi Bukoba wajawazito wawili walikwenda kupata huduma ya kujifungua hospitali, anaambiwa mlinzi waite manesi, mlinzi anasema ‘nesi amesema nisifungue mlango’.

“Mwambie kuna kinamama wanataka kujifungua, ‘nesi amesema nisifungue mlango’ mpaka wakajifungulia getini kwa hivyo dharau hizi, uzembe huu, kutokuwa na usimamizi wa kutosha kunaleta maafa kwa wanawake wakati wa kujifungua.

“Ninadhani hatupaswi kupata hukumu hii, ingawa mwisho yakitokea tunasema Mungu ndivyo alivyoandika, kusingekuwa na uzembe Mungu asingeandika, waziri na watu wako msimamie hayo mambo kwenye vituo vya kutoa huduma.”

WAKUU MIKOA KUPIMWA

Kuhusu lishe bora na huduma ya mama na mtoto, Rais Samia alimweleza Waziri wa Afya kuwa kuna haja ya kuingia tena mikataba na wakuu wa mikoa kulifufua na atakayeshindwa kufikia vigezo hafai kuwapo kwenye mkoa.

Mkurugenzi Mtendaji Mkuu CCBRT, Brenda alimwahidi Rais kuwa watafanya kila liwezekanalo waendelee kutoa huduma bora.

Waziri Ummy alimpongeza Mwenyekiti wa Bodi ya hospitali hiyo, Dk. Wilbroad Slaa kwa kuisimamia hospitali hiyo na Mkurugenzi ambaye sio daktari kitaaluma, lakini anafanya vizuri.

Mlezi wa hospitali hiyo, Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, aliomba wadau wengine waunge mkono juhudi zilizofanywa kwa kupeleka fedha ili kuwasaidia Watanzania wanaofika kutibiwa.

Mwakilishi wa wadau wa maendeleo wa CCBRT, Balozi wa Ujerumani nchini, Regine Hess, alisema jengo hilo ni muhimu kwa sababu lina mchango mkubwa wa kukuza usawa wa kijinsia ambao Tanzania imefikia kiwango cha juu.

Habari Kubwa