Rais Samia aonya nidhamu ya uwoga

22May 2022
Paul Mabeja
Dodoma
Nipashe Jumapili
Rais Samia aonya nidhamu ya uwoga

​​​​​​​RAIS Samia Suluhu Hassan, ameonya tabia ya baadhi ya watumishi wa umma kuwa na nidhamu ya uwoga badala yake wafanye kazi kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu.

Rais, Samia Suluhu Hassan akimuapisha. Balozi, Adadi Rajabu, kuwa Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Umma katika hafla fupi iliyofanyika Ikulu Chamwino Jijini Dodoma jana. PICHA: IKULU

Amesema nidhamu kwa baadhi ya watumishi wa umma inakuwapo pale tu wanapotiwa vitisho lakini vitisho vikiondoka, nidhamu hiyo nayo inatoweka.

Rais Samia alibainisha hayo jana Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma baada ya kuwaapisha viongozi mbalimbali aliowateua, wakiwamo wa Tume ya Utumishi wa Umma.

“Watumishi wetu hawajielewi. Nidhamu yao mpaka wapate vitisho, wakipata vitisho nidhamu inakuwepo, vitisho vikiondoka nidhamu hakuna.

“Sasa tunataka watumishi ambao watakuwa wana itikadi moyoni mwao kuwa mimi ni mtumishi wa umma ‘ethics’ (maadili) zangu (yangu) ni hizi. Nidhamu  yangu mstari ni huu hapa,” alisisitiza Rais Samia.

Kutokana na hali hiyo, aliitaka Tume ya Utumishi wa Umma wakalisimamie sana suala la nidhamu kwa watumishi pamoja na mambo ya kimuundo.

Pia alisema hali ya kushuka kwa nidhamu kwa watumishi inatokana na kutokuwapo na mafunzo ya mara kwa mara ya kada mbalimbali za utumishi wa umma.

“Nakumbuka mimi na Haule tulivyokuwa IDM (Mzumbe)  kila baada ya muda tulikuwa tunaona makatibu wakuu, wakurugenzi kina nani walikuwa wanaingia pale na wana mabweni yao maalum. Sisi hatusogei huko, tunasema wakubwa wameingia. Walikuwa  wanakuja na kuondoka, wanapata kozi fupifupi za mafunzo za kuwakumbusha wajibu wao wakiwa kazini.

“Jambo ambalo kwa muda mrefu limekufa lilikuwa linaendelezwa kidogo kidogo lakini baadaye likaachwa kabisa. Kwa maana hiyo, watumishi wa umma wamejikalia tu, wanakwenda tu, wanapandishwa vyeo bila kupata mafunzo yoyote yale. Kwa hiyo watu wanakwenda tu, naomba mkalisimamie sana suala hili,” alisema.

Pia alisema Tume ya Utumishi inao wajibu wa kuhakikisha inarudisha nidhamu katika utumishi wa umma na uwajibikaji.

“Kwa sababu mtu unamwongezea tu mavyeo bila kumpa mafunzo, juzi wamefurahi wamepanda vyeo kwa mseleleko lakini huo mseleleko maana yake hawajui. Mtu  kapanda ngazi mbili hadi tatu kwa pamoja lakini wajibu wake nini? Anapokwenda hajui, naomba myasimamie sana sana,” alisisitiza.

Vilevile, aliitaka Tume ya Utumishi kwenda kusimama katikati bila upendeleo kwa kuwa Watanzania wote ni sawa na wenye sifa pekee ndiyo watatakiwa kwenda.

Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, akizungumza katika hafla hiyo, alimpongeza Rais Samia kwa kupandisha mishahara ya watumishi.

Alisema Bunge ambalo kazi yake ni kuisimamia na kuishauri serikali, linampongeza Rais kwa kusikia kilio cha watumishi ambacho kimekuwepo kwa muda mrefu.

“Mheshimiwa Rais, sisi kama Bunge tunatoa pongezi zetu kwako kwa hatua hii uliyoichukua ambayo hata sisi tumekuwa tukiizungumzia kama wawakilishi wa wananchi ni jambo kubwa sana sana na tunakupongeza sana,” alisema Dk. Tulia.

Pia alimpongeza kwa kuitangaza nchi kupitia filamu ya Royal Tour ambayo inawezesha kukua kwa sekta ya utalii nchini na kuliongezea taifa mapato.

“Lakini Mheshimiwa Rais ulipokuwa kwenye ziara yako ya kikazi Tabora hivi karibuni ulipata mapokezi makubwa sana hali hii inamaanisha kuwa watanzania wengi wanaguswa na namna unavyo fanya kazi yako hasa katika miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya barabara”alisema

Hata hivyo, alisema Bunge linaendelea na jitihada za kutoa elimu kwa wabunge ili kuondoa migogoro iliyopo baina ya wabunge na wakurugenzi.

“Mheshimiwa hili ulishatoa maagizo lakini sisi kama bunge lazima pia tutoe elimu kwa wabunge wetu ili kila mmoja afanye kazi yake bila kumwingilia mwingine. Lakini  pia tunaendelea kuisimamia na kuishuri serikali kama ilivyo wajibu wetu,” alisema.

Habari Kubwa