Rais Samia awakumbuka machinga

17May 2022
Paul Mabeja
DODOMA
Nipashe
Rais Samia awakumbuka machinga

RAIS Samia Suluhu Hassan, amesema katika mwaka wa fedha unaoanza Julai mwaka huu, ofisi yake itatoa Sh. milioni 10 kwa kila mkoa kuwezesha shughuli za machinga nchini.

RAIS Samia Suluhu Hassan.

Rais Samia alibainisha hayo jana kwa njia ya simu baada ya kupiga moja kwa moja na kuzungumza na wamachinga waliohudhuria mkutano wa mafunzo ya viongozi wa Machinga nchini (SHIUMA).

Mafunzo hayo yanafanyika jijini hapo kwa siku tano yakihusisha viongozi wa Machinga Tanzania Bara na Visiwani.

“Nakushukuru Waziri kwa kuwapa machinga ofisi katika jengo la serikali, nimefuatilia risala yenu na nimefurahishwa nawahakikishia ushirikiano na mazingira mazuri na ifikapo mwaka wa fedha unaoanza mwezi Julai mwaka huu Ofisi ya Rais itatoa milioni 10, kwa kila mkoa kuwezesha shughuli za kuendesha ofisi za machinga mkoa," alisema Rais Samia.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk. Dorothy Gwajima, alimpongeza Rais Samia kwa uamuzi huo ambao alisema umeleta tumaini jipya kwa machinga nchini.

Aliwataka machinga kuhakikisha kuwa fedha hizo haziwi chanzo cha kuvuruga umoja wao badala yake wazitumie kwa kazi iliyokusudiwa na kuwapo uwazi utakaoonyesha zimetumika kwa matumizi gani.

Pia, alimwagiza Katibu Mkuu wa wizara yake kuwakutanisha machinga na taasisi za fedha nchini ili kujadiliana namna ya kupunguza riba za mikopo kwa kundi hilo.

“Kama mheshimiwa Rais amewaahidi na kuwapatia kiasi hicho cha fedha kwanini taasisi za fedha zisione umuhimu wa kukaa meza moja na kundi hili kubwa ili kupunguza riba za mikopo na kuwawezesha mitaji,” alisema Dk. Gwajima.

Kadhalika, alimwagiza Katibu Mkuu kufanya utafiti utakaosaidia serikali kujibu kero za kundi hilo badala ya kuendelea kufanya vitu kimazoea.

Vilevile, aliwataka machinga nchini kuhakikisha kuwa wanashiriki kikamilifu sensa ya watu na makazi inayotarajiwa kufanyika Agosti 23, mwaka huu.

“Mnapaswa kujitokeza kuhesabiwa ili kuiwezesha serikali kupata takwimu sahihi tusiwe tunasema mpo milioni tatu kumbe mpo milioni sita hivyo wote mjitokeze kuhesabiwa,” alisema.

Awali, Naibu Katibu Mkuu (SHIUMA), Joseph Mwanakijiji, alisema uhusiano mzuri walionao hivi sasa na serikali unasaidia machinga kuwa na mazingira mazuri na kufanya biashara kwa uhuru.

"Tuna changamoto nyingi, lakini kero ya miundombinu kwa baadhi ya masoko haiko sawa na kusababisha kiuchumi hatufikii malengo, baadhi ya miundombinu haiko sawa na kuhatarisha afya, ukosefu pia wa ofisi za machinga na changamoto za kibajeti," alisema.

Alizitaja changamoto nyingine kuwa ni pamoja na stadi za biashara, makazi bora, umilikishwaji wa maeneo ya machinga na kuomba kupewa barua ya idhini kuepuka kuondolewa mara kwa mara yanapotokea mabadiliko.

Habari Kubwa