Rais Shein atoa msamaha kwa wafungwa 12

13Jan 2018
Rahma Suleiman
Nipashe
Rais Shein atoa msamaha kwa wafungwa 12

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ametoa msamaha kwa wafungwa 12 ikiwa ni miongoni mwa sherehe za miaka 54 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein akipungia mkono wananchi, wakati akiwasili katika uwanja wa Abeid Amani Karume mjini Unguja jana, katika sherehe za Miaka 54 ya Mapinduzi ya Zanzibar. PICHA: IKULU

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, Dk. Abdulhamid Yahaya Mzee, ilieleza kuwa kwa uwezo aliopewa chini ya kifungu cha 59 cha Katiba ya Zanzibar 1984, Rais ameamuru kuwa kifungo kilichobaki cha wanafunzi walionufaika na msamaha huo, ambao bado wanaendelea kutumikia katika vyuo vya mafunzo vya Unguja na Pemba kuwa kipindi hicho chote kinafutwa na kwamba wanafunzi hao waachiwe huru kuanzia Januari 11, 2018.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa, kwa kuwa Zanzibar itakuwa inasherehekea miaka 54 ya Mapinduzi ya Zanzibar Januari 12, 2018, na kwa kuwa Rais ameridhika kuwa kuna sababu za kutosha za kutumia uwezo wake huo katika sherehe hiyo, wanafunzi hao waachiwe huru.

Walionufaika na msamaha huo kwa Unguja ni Abdul-Azizi Abdalla Mohamed, Omar Abdalla Nuhu, Ali Khamis Mrau, Mussa Ali Vuai, Hassan Seif Khamis, Nassor Abeid Issa, Jihadi Jalala Jihadi na Edward Jeremia Magaja. Aidha, wengine walionufaika na msamaha huo kwa upande wa Pemba ni Suleiman Abdalla Amir, Mtumwa Khamis Kaimu, Said Seif Omar na Masoud Seif Nassor.

Wakati huohuo,  Dk. Shein amewavisha Nishani ya Mapinduzi na Nishani ya Utumishi uliotukuka watunukiwa 74.Hafla hiyo imefanyika katika viwanja vya Ikulu mjini Zanzibar ambayo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa vyama na serikali pamoja na wananchi.

Nishani ya Mapinduzi hutolewa kwa mtu ambaye aliasisi au alishiriki au aliyatukuza na aliyaenzi Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 na mtunukiwa huwa ni kiongozi au mtu mwingine aliye hai au aliyefariki ambaye aliiletea sifa Zanzibar katika fani mbalimbali na kuonyesha maadili mema ya kusifika na kuigwa.

Nishani ya Utumishi uliotukuka inatolewa kwa mtumishi wa umma au Idara Maalumu za SMZ aliye hai au aliyefariki ambaye ametimiza utumishi wake kwa muda wa miaka isiyopungua 20 mfululizo na kwa mtumishi wa Idara Maalumu za SMZ miaka isiyopungua 20 ya kuwa ofisa na katika kipindi chote hicho amekuwa na tabia njema.

Mtumishi huyo awe ametumikia taifa kwa uzalendo wa hali ya juu na kufanya kazi kwa kujitolea, uwajibikaji, uadilifu, ujasiri na umakini katika kusimamia majukumu na utendaji kazi.

Waliovishwa Nishani ya Mapinduzi ni Jaji Augustino Ramadhan, Marehemu  mstaafu Juma Abdalla Saddala (Mabodi),  Ramadhan Abdalla Shaaban,  Ali Ameir Mohammed, Ali Mohammed Shoka, Marehemu Kassim Ali Kassim, Rajab Baraka Juma, Khamis Ahmada Mussa, Marehemu Dk. Ishau Abdalla Khamis. Wengine ni Ali Salum Ahmed, Shema Mohamed Sheha, Issa Mohamed Suleiman, Enoch Timoth Bilal,  Fatma Said Ali, Damian Z. Lubuva, Mwalimu Haji Ameir, Mbarouk Rashid Omar, Issa Ahmed Othman, Mohamed Khamis Abdalla, Abdulsalam Issa Khatib, Marehemu Christabella Susan Majaaliwa, Marehemu Shaha Kombo Shaha, Amina Said Ferouz. Ramadhan Abdalla Ali.

Aidha, Abdulrahman Mwinyi Kombo, Hassan Mussa Takrima, Zaina Khamis Rashid, Mosi Jecha Pili,  Maulid Salum Abdalla, Haji Machano Haji, Marehemu Rajab Kheir Yussuf, Said Matar Mwinyi, Salum Nassor Said.

Miongoni mwa waliovishwa nishani ya utumishi ni Othman Bakar Othman, Sheikh Harith Bin Khelef, Ramadhan Hamad Hilika,Mkadam Juma Nassib, Saleh Sadik Osman, Juma Khiari Simai, Kassim Maalim Suleiman. 

 

Habari Kubwa