Rais Uhuru mgeni rasmi siku ya uhuru

04May 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Rais Uhuru mgeni rasmi siku ya uhuru

Rais Samia Suluhu Hassan, amesema amemualika Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta, kuwa mgeni rasmi ifikapo Desemba 9, mwaka huu wakati Tanzania itakapoadhimisha miaka 60 ya uhuru iliyoupata kutoka kwa Waingereza.

Samia ameyasema hayo leo Mei 4, 2021 katika Ikulu ya Nairobi nchini Kenya, kwenye ziara ya siku mbili yenye lengo la kukuza uhusiano kati ya Tanzania na Kenya kufuatia mualiko wa Rais Uhuru.

“Ifikapo Desemba mwaka huu Tanzania itatimiza miaka 60 ya uhuru wetu hivyo nimetoa mualiko rasmi kwa Rais Uhuru Kenyatta awe mgeni rasmi katika maadhimisho hayo,” amesema Samia.

Katika mazungumzo hayo wamekubaliana mambo kadhaa ikiwamo kukuza na kuimarisha uhusiano na mshikamano baina ya mataifa hayo.

"Tumekubaliana kuendelea kushughulikia baadhi ya changamoto hususan vikwazo visivyo vya kodi ambavyo vinatokea katika mipaka yetu tumekubaliana sasa vindoke na kwa pamoja tumeitaka tume yetu ya ushirikiano baina ya Kenya na Tanzania iwe inakaa na kutoa suluhu ya vikwazo vinavyojitokeza hivi sasa ,” amesema.

Wakuu hao wa nchiz hizo mbili wamekubaliana pia mawaziri wa afya kukutana mara kwa mara kwajili ya kuangalia namna bora ya kurahisisha mfumo wa upimaji wa ugonjwa wa corona na watu waendelee kufanya biashara zao kama ilivyokuwa hapo awali.

“Jambo lingine ambalo Rais Kenyatta ameongezea na mimi nakubaliana naye ni kwamba mawaziri wetu wa afya kukaa na kuangalia namna ya kurahisisha mfumo wa kuingia na kupimwa kwenye mambo haya ya corona ili watu waweze kupita na biashara ziendelee,” ameongeza Samia.

“Tumekubaliana kuhusu namna ya kukuza biashara na uwekezaji kati yetu kama mnavyofahamu nchi zetu zina fursa nyingi sana ikiwemo kwenye kilimo, viwanda, uvuvi na utalii Mungu ametupendelea hivyo tunakwenda kuzitumia fursa hizi kukuza biashara kati yetu na mataifa ya nje,”

“Mbali na uwekezaji nchi za Tanzania na Kenya ni wadau wakubwa wa biashara ambapo kwenye miaka mitano iliyopita wastani wa biashara kati ya nchi hizi ni Dola za Kimarekani milioni 450 ambayo bado sio kubwa na tumeweka ahadi kuikuza,”

Kwa upande wake, Rais Uhuru amesema tayari nchi hizo mbili zimeweka mikataba ya ujenzi wa bomba la gesi kutoka Dar es Salaam hadi Mombasa pamoja na ule wa mkataba wa kuimarisha utamaduni na utalii.

"Tumeweka mikataba hasa kuhusu pipeline ya gas toka Mombasa hadi Tanzania. Pia tumeweka mkataba wa kuimarisha culture and national heritage, mkataba wa tourism," amesema Uhuru.

"Tumepata nafasi ya kuongea…Tumekubaliana mawaziri wetu wawe na mazungumzo ili kuboresha mahusiano kati ya nchi zetu, kurahisisha mahusiano na biashara kati ya nchi zetu mbili," amesema.

Habari Kubwa