Rais wa Simba alazwa ICU

09Mar 2018
Hellen Mwango
Nipashe
Rais wa Simba alazwa ICU

UPANDE wa utetezi katika kesi ya kutakatisha dola za Marekani, 300,000 inayomkabili Evance Aveva na mwenzake jana uliiambia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa mshitakiwa huyo ameshindwa kufika mahakamani kwa kuwa bado mgonjwa na amehamishiwa wodi ya wagonjwa mahututi (ICU) tangu juzi.

Mbali na Aveva ambaye ni rais wa klabu ya michezo ya Simba ya jijini Dar es Salaam, mshtakiwa mwingine ni Godfrey Nyange 'Kaburu'.

Kaburu ambaye ni makamu wa rais wa Simba jana alisimama mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri kusikiliza kesi hiyo iliyopangwa kwa ajili ya kutajwa.

Zaidi ya mwezi mmoja sasa upande wa utetezi umekuwa ukiijulisha mahakama kwamba mshtakiwa huyo amelazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa ajili ya matibabu na kwamba ameshindwa kufika mahakamani kusikiliza kesi yake.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Leonard Swai alidai kuwa upelelzi wa kesi hiyo bado haujakamilika na amepokea taarifa kwamba mshtakiwa wa kwanza bado mgonjwa.

“Mheshimiwa hakimu, Aveva tangu jana (Jumatano) amehamishiwa wodi ya wagonjwa mahututi kutokana na hali yake kuzidi kuwa mbaya… “ alidai wakili wa utetezi, Evodius Mtawala.

Katika kesi ya msingi, vigogo hao wanakabiliwa na mashtaka matano ya kughushi, kuwasilisha nyaraka ya uongo na kutakatisha dola 300,000.

Katika shtaka la kwanza ilidaiwa mahakamani hapo walipopanda kizimbani kwa mara ya kwanza Juni 29, mwaka jana kuwa Machi 15, 2016 washtakiwa wote kwa pamoja walighushi fomu ya kuhamisha fedha ya tarehe hiyo wakionyesha kwamba klabu ya Simba inalipa deni la dola za Marekani 300,000 kwa rais wake Aveva.

HAMISHA FEDHAKatika shtaka la pili, ilidaiwa kuwa Machi 15, 2016 katika benki ya CRDB tawi la Azikiwe lililopo Ilala, jijini Dar es Salaam, Aveva aliwasilisha fomu ya kuhamisha fedha zilizoghushiwa ya terehe hiyo akionyesha kwamba Klabu ya Simba imemlipa dola za Marekani 300,000 huku akijua sio kweli.

Msigwa alidai katika shtaka la tatu, kati ya Machi 15 na Julai 29, 2016, washtakiwa wote wawili walikula njama ya kutakatisha fedha hizo huku wakijua zimetokana na nyaraka za kughushi.

Upande wa Jamhuri ulidai katika shtaka la nne, Machi 15, 2016 katika benki ya Barclays Tanzania Limited, tawi la Mikocheni, Wilaya ya Kinondoni Aveva alihamisha dola za Marekani 300,000.

Shtaka la tano, ilidaiwa kuwa Machi 15, mwaka 2016 katika benki ya Baclays tawi la Mikocheni, Kaburu alimsaidia Aveva kupata dola za Marekani 300,000 wakati akijua zimetokana na zao la uhalifu.

Washtakiwa wote walikana mashtaka yao lakini kwa kuwa mashtaka ya kutakatisha fedha hayana dhamana kwa mujibu wa sheria, walinyimwa.