RC aeleza sababu umaskini Simiyu

05Jul 2019
Happy Severine
BARIADI
Nipashe
RC aeleza sababu umaskini Simiyu

MKUU wa Mkoa wa Simiyu, Antony Mtaka, ameeleza sababu za mkoa huo kushika nafasi ya pili kutoka mwisho katika mikoa inayoongoza kwa kiwango cha umaskini wa kipato Tanzania Bara.

MKUU wa Mkoa wa Simiyu, Antony Mtaka.

Amesema sababu kubwa ya kufikia hatua  hiyo ni kutokuwapo kwa mwamko wa elimu kwa wananchi tangu zamani na kufanya idadi kubwa ya wananchi wasio na   elimu.

Mtaka alisema hayo jana wakati akizungumza na madiwani wa Halmashuari ya Wilaya ya Bariadi kwenye kikao cha baraza kujadili taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kilichofanyika mjini hapa.

Alisema bila wananchi wa mkoa na viongozi wote kubadilika na kuwekeza katika elimu, Simiyu itaendelea kushika nafasi za mwisho kwa umaskini wa kipato.

Kiongozi huyo alisema mikoa yote ambayo imeongoza kwa kiwango kidogo cha umaskini, imewekeza katika elimu huku zikiwako shule nyingi za kidato cha tano na sita pamoja na vyuo.

"Lazima tuwekeze sana katika elimu, bila ya kufanya hivyo hatuwezi kuvuka hapa. Lazima watu wabadilike, elimu ndiyo kila kitu. Hizi nguvu ambazo tunazifanya hapa hazitafanikiwa kama tutakuwa na watu ambao hawana elimu," alisema.

"Watu wanatakiwa kubadilika na kuona elimu ndiyo mkombozi wa maisha yetu, tuachane na mila potovu, kuozesha watoto katika umri mdogo, kuwakatisha masomo na kuwaozesha,” aliongeza.

Mkuu huyo wa mkoa aliwataka viongozi kuungana na serikali katika juhudi zake za kuongeza shule nyingi za kidato cha tano na sita na vyuo mbalimbali vya ufundi na taaluma.

Hivi karibuni, Ofisi ya Taifa Takwimu (NBS) ilitoa takwimu za mikoa yenye kiwango cha umaskini na kipato zilizoonyesha kuwa mkoa wa Simiyu umeshika nafasi ya pili kutoka mwisho ukiwa na asilimia 39.2 nyuma ya Rukwa wenye asilimia 45.