RC ageukia usafi Jiji Dodoma

05Aug 2020
Na Mwandishi Wetu
Dodoma
Nipashe
RC ageukia usafi Jiji Dodoma

MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Binilith Mahenge, ametoa siku 14 kwa Jiji la Dodoma kukaa na kampuni na vikundi vya usafi ili kuweka mkakati mahususi wa uzoaji taka kutokana na kukithiri kwa uchafu kwenye masoko.

Dk. Mahenge alisema hayo jana katika mkutano na wafanyabiashara pamoja na watendaji wa jiji, maofisa afya, taasisi za serikali, viongozi wa masoko na vikundi vya usafi, jijini hapa.

Alisema kuna malalamiko ya wafanyabiashara kuhusu kukithiri uchafu katika masoko ya jiji na kutoa wiki mbili kushughulikiwa suala hilo.

“Taasisi hizi zinatakiwa kukutana na kuweka azimio namna bora ya kuzoa taka katika jiji hili, ili wafanyabiashara kufanya kazi zao katika mazingira safi na salama kwa afya zao na wateja wao.

“Jiji linatakiwa kujadiliana na Kampuni ya Usafi ya Green Waste, vikundi vya usafi na viongozi wa masoko jijini ili kuweka utaratibu mzuri wa kuzoa taka na kuondoa kero ya kujaa taka katika maeneo mbalimbali jijini,” alisema Dk. Mahenge.

Pia aliagiza kuangalia mkataba wa kampuni hiyo kama ina uwezo wa kuzoa taka na kama ina uwezo ianze kufanya kazi hiyo usiku badala ya mchana.

“Iundwe kamati ya kufuatilia masuala ya usafi unavyofanyika katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dodoma kutokana na kile kinachoonekana kuwa Kampuni ya Green Waste imeshindwa kutokana na kuzidiwa na kazi na kukosa vifaa vya kutosha,” alisema.

Naye Mkurugenzi wa Jiji hilo, Godwin Kunambi, alibainisha kuwa kampuni hiyo inazoa taka katika kata za Uhuru, Madukani, Majengo, Viwandani, Kilimani, Tambukareli, Makole na Kiwanja cha Ndege na kata hizo zinazalisha tani 38 za taka kwa siku.

Kunambi alisema katika kudhibiti utupaji taka holela mitaani mzabuni huyo ameweka makasha makubwa 20 na jiji pia limeweka pia makasha 20 kwa ajili ya kuhifadhi taka kabla ya kuondolewa na kusafirishwa kwenda dampo.

“Katika usafi wa mazingira Jiji la Dodoma tuna vikundi 96 ambavyo kutokana na uwezo kidogo vinatakiwa kukusanya taka na kufikisha kwenye mapipa makubwa yaliyopo mjini na kampuni hiyo inatakiwa kufikisha dampo,” alisema.

Ofisa Afya Msafirishaji Taka katika Jiji la Dodoma, John Lugendo, alisisitiza kuwa wafanyabiashara wanatakiwa kujua kwamba sheria ndogo ya jiji inataka taka za majani ya migomba zinatakiwa kusafirisha na wao hadi dampo isipokuwa taka nyingine.

Kaimu Ofisa Afya wa Jiji hilo, Ally Mfinanga, alisema kwa sasa Halmashauri ya Jiji inatumia zaidi ya Sh. milioni 25 kwa mwezi kwa ajili ya mafuta ya magari kupeleka taka dampo.

Habari Kubwa