RC agoma kuachia uenyekiti wa CCM

10Aug 2018
Nebart Msokwa
MBEYA
Nipashe
RC agoma kuachia uenyekiti wa CCM

MKUU wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila amesema hatajiuzulu nafasi ya Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa  licha ya kushinikizwa na baadhi ya wanachama kuachia nafasi hiyo.

MKUU wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila.

Chalamila alitoa msimamo huo jana alipokuwa anazungumza na viongozi wa dini na kueleza baadhi ya wanachama wa CCM Mkoa wa Iringa wanamshinikiza ajiuzulu, ili kukidhi matakwa ya utaratibu mpya wa chama unaotaka mtu mmoja kuwa na cheo kimoja.

Alisema ataendelea kuwa mwenyekiti mpaka Rais Dk. John Magufuli ambaye ndiye aliyemteua, atakapotoa maelekezo mengine.

“Baada ya kuteuliwa kuna baadhi ya watu walinifuata wakinitaka nijiuzulu nafasi ya uenyekiti, sasa ninachokijua ni kwamba Rais aliniteua kuwa Mkuu wa Mkoa akiwa anajua kuwa mimi ni mwenyekiti, hivyo anaendelea kushika nyadhifa zote mpaka nitakapopata maelekezo mengine,” alisema Chalamila.

Katika hatua nyingine, Chalamila alisema kwa muda mrefu Jiji la Mbeya limekuwa halipati maendeleo kutokana na mwendelezo wa siasa chafu zinazoifanya serikali ishindwe kutekeleza baadhi ya miradi ya maendeleo.

Aliwataka viongozi wa dini kuisaidia serikali katika kuhubiri amani na kuwaelimisha vijana kufanya kazi kwa bidii badala ya kuendekeza vijiwe vya siasa zisizokuwa na manufaa katika maisha yao ikiwamo kukashifu vyama wasivyoviunga mkono.

Alisema katikati ya Jiji la Mbeya barabara ilitakiwa iwe ya njia nne na barabara ya mchepuko kutoka Uyole mpaka Songwe kwa ajili ya magari makubwa ya mizigo ilitakiwa iwe imejengwa, lakini siasa zimekuwa zikikwamisha.

“Hili ni jiji, lakini siku zote huwa najiuliza kuwa ni kweli serikali imeshindwa kujenga barabara ya njia nne, ni kweli serikali imeshindwa kujenga kilomita 40 barabara ya mchepuko na je, serikali imeshindwa kuukamilisha uwanja wa ndege wa Songwe na kuupa hadhi yake ya kimataifa?” Alihoji Chalamila.

 

“Ninachokiona hapa ni kwamba siasa ndiyo ‘zinatucost’ (zinatugharimu), mtu anaamua kurudisha nyuma mikono na kuacha aone tunavyofanya, lakini kwa sasa naona hali imeanza kuwa tulivu, mimi na katibu tawala tutamwandikia rais atusaidie baadhi ya miundombinu hii muhimu iboreshwe haraka,” alisisitiza.

Aliwaomba viongozi wa dini mkoani humo, kuendelea kuisaidia serikali kuwaelimisha vijana kuhusu mambo mbalimbali ya maendeleo na kuachana na siasa chafu ambazo hazina manufaa kwa sasa.

Aliwataka kuanzisha madarasa maalumu ya kuwafundisha vijana ujasiriamali kwenye maeneo yao ya kuabudia, ili wajikite kwenye shughuli hizo na kujiletea maendeleo.

Kwa upande wao baadhi ya viongozi hao wa dini walikiri siasa kuwa kikwazo kwa maendeleo ya Jiji la Mbeya hivyo wakamuomba Mkuu huyo wa Mkoa kuwakutanisha na viongozi wa vyama vya siasa ili kujadiliana namna ya kukomesha siasa hizo.

Mmoja wa viongozi hao, Mchungaji Shell Goratan, alisema mara nyingi wanasiasa wa mkoa huo wamekuwa wakiangalia maslahi yao binafsi badala ya kuangalia ya wananchi.

Alisema Mkoa wa Mbeya umekuwa ukiingiliwa zaidi na wanasiasa hata katika utendaji wake wa kazi na kusababisha kushindwa kuendelea kama mikoa mingine.

Alisema mara nyingi wanasiasa hao wamekuwa wakiingiza siasa zao hadi kwenye miradi ya maendeleo na hivyo kukwamisha shughuli hizo zisiendelee.

“Sisi tupo tayari kuisaidia serikali katika kukemea mambo haya yanayotusumbua siku zote, tutahakikisha tunahubiri maendeleo ya mkoa wetu ili tupate maendeleo kama mikoa mingine,” alisema Goratan.

Kwa upande wake Shekhe Hassan Katanga, alisema kufuatia tatizo la siasa katika mkoa huo, wako tayari kuanza kutoa elimu kwa vijana ili kuwatoa vijiweni na kuingia kwenye ujasiriamali.

 

Alisema ikiwezekana wataomba vibali vya kuanza kutoa elimu hiyo hadi kwenye taasisi za elimu ikiwamo shule za sekondari.

Habari Kubwa